Merkel: Kujitenga sio jibu la matatizo
24 Januari 2018Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema suala la kujitenga sio jibu la kutatua matatizo na changamoto za kiuchumi zinazoikabili dunia. Merkel amesema pia soko la pamoja ni kipaumbele kikubwa cha Ulaya.
Akizungumza leo katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa mjini Davos, Uswisi, Kansela Merkel amesema kuwa yuko wazi kuhusu aina ya ushirikiano ambao Umoja wa Ulaya utauendeleza baada ya Uingereza kujiondoa katika umoja huo. Hata hivyo, amesema kwamba huenda pasiwepo na maelewano kuhusu kanuni za msingi za Umoja wa Ulaya katika mazungumzo hayo. Amesema wanataka ushirikiano wa karibu na Uingereza.
''Ujerumani inapenda kuwa nchi ambayo itatoa mchango wake, pia katika siku zijazo katika kutatua kwa pamoja matatizo ya dunia. Tunadhani kujitenga na wengine duniani hakutatuongoza na kutupeleka katika mustakabali mzuri. Kujitenga sio jibu sahihi,'' alisema Merkel.
Merkel pia amesema siasa za kizalendo zinazofanywa na wanasiasa wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya ni ''sumu'' ambayo ianchangia katika matatizo ambayo hayatatuliki. Amesema ana matumaini kwamba vyama vyenye msimamo huo havitaongezeka na kwamba serikali yake inajaribu kukidhibiti chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji, AfD, ambacho kilishindwa viti bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Septemba. Amesema vyama hivyo vimeshika kasi pia Ufaransa, Uholanzi na kwengineko.
Kansela Merkel amezungumza kabla ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambaye anatarajiwa kuzunguzmia kuhusu hali ya sasa ya utandawazi na changamoto tatu zinazoikabilia dunia ambazo ni kutofautiana kwa usawa katika uchumi na masuala ya kijamii, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uongozi wa dunia katika nyanja ya uzalend o na itikadi kali.
Gentiloni aonya sera ya Trump kujitenga
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni leo ameonya kuwa hamu ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuiweka ''Amerika Kwanza'' ni halali, lakini suala la kujitenga halina faida. Akizungumza na waandishi habari mjini Davos, Gentiloni wanachohitaji ni ukuaji wa uchumi na ustawi na kuwalinda wafanyakazi wao.
Ama kwa upande mwingine, Mfalme wa Uhispania, Felipe wa Sita amesema shinikizo la uhuru wa jimbo la Catalonia ilikuwa ni shambulizi dhidi ya mfumo wa demokrasia ya nchi hiyo na inapaswa kutumika kama somo la demokrasia duniani kote ili kuheshimu utawala wa sheria na uhuru wa kitaifa. Akizungumza katika kongamano hilo, Mfalme Felipe amesema kilichotokea Catalonia kilikuwa jaribio la kukandamiza kanuni za msingi za mfumo wa demokrasia.
Aidha, Trump ambaye atalihutubia kongamano hilo siku ya Ijumaa anatarajiwa kuitumia ziara yake hiyo barani Ulaya kama fursa ya kufanya mazungumzo na washirika wake wa kisiasa. Trump amepangiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa Rwanda, Paul Kagame pamoja na mwenyeji wa kongamano hilo, Rais wa Uswisi, Alain Berset, huku mazungumzo yao yakitarajiwa kuangazia masuala ya kichumi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman