1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Marekani, kukutana na Biden

15 Julai 2021

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameelekea Marekani kama sehemu ya ziara yake rasmi za mwisho kabla ya kuondoka madarakani, ambapo siku ya Alhamisi anatarajiwa kukutana na Rais Joe Biden.

Bildkombo Angela Merkel und Joe Biden

Merkel na Biden watazungumzia masuala kadhaa ikiwemo kuimarisha uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani, janga la virusi vya corona, China pamoja na mradi wa bomba la gesi unaogharamiwa na Urusi na Ujerumani unaojulikana kama Nord Stream 2. Kwa muda mrefu serikali ya Marekani imekuwa ikiupinga ujenzi wa mradi huo, ikisema utadhoofisha usalama wa nishati barani Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas ambaye tayari yuko Marekani amewaambia waandishi habari kwamba nchi hizo mbili zimekubaliana masuala kadhaa kuhusu mradi huo. Lakini amesema bado haijafahamika iwapo tofauti zilizopo zitatafutiwa ufumbuzi wa kudumu katika ziara hii ya Merkel.

Ingawa Kansela Merkel ameizuru Marekani zaidi ya mara 20 katika uongozi wake wa miaka 16, hii ni ziara ya kwanza katika Ikulu ya Marekani katika kipindi cha miaka mitatu. Pia atakuwa kiongozi wa kwanza wa Ulaya kuitembelea Marekani tangu Biden alipoingia madarakani.

Mwanzo mpya

Ziara ya Merkel inaashiria mwanzo mpya katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili baada ya kuwepo kwenye mvutano na serikali ya Donald Trump. Cathryn Clüver Ashbrook, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Ujerumani linalohusika na Uhusiano wa Kigeni anasema uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani ni wa muda mrefu sana.

''Tusisahau kwamba Angela Merkel ni mmoja kati ya marafiki wazuri wa Marekani. Ukipima tu ukweli kwamba aliyahutubia mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani, kwamba alitunukiwa Medali ya Uhuru na kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Chuo Kikuu cha Havard miaka michache iliyopita. Hivyo nadhani katika Ikulu ya Marekani na rais wa sasa, anaonekana kama ngao thabiti ya uhusiano wa kisasa kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani,'' alifafanua Ashbrook.

Wanaharakati wakiwa wamevalia sura za Merkel na Biden na ujumbe wa kuondolewa hati miliki ya chanjo ya COVID-19Picha: picture alliance/dpa

Kulingana na duru za serikali ya Marekani, Merkel na Biden pia watazungumzia kitisho cha mabadiliko ya tabia nchi na kukuza ustawi wa uchumi na usalama wa kimataifa. Merkel atakutana pia na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, maafisa wengine wa ngazi ya juu wa nchi hiyo pamoja na wafanyabiashara wa Marekani.

Baada ya kufanya kazi na Merkel kwa miaka 16, maafisa wengi wa Marekani na kwengineko duniani hawaelewi Ujerumani itachukua hatua gani baada ya uchaguzi wa kansela Septemba 26. Akiwa madarakani, Merkel amefanya kazi na marais wanne wa Marekani.

Maandamano ya wanaharakati

Kabla ya ziara ya Merkel siku ya Jumatano wanaharakati kadhaa waliandamana mjini New York kupinga hatua ya Ujerumani kutounga mkono mpango wa kuondoa hati miliki ya chanjo ya COVID-19, wakati Marekani inaunga mkono. Madaktari wasio na mipaka wamemtaka Merkel kuachana na mpango wake huo.

Wakati huo huo, Chama cha Waandishi Habari nchini Ujerumani, DJV kimemsihi Merkel kumshawishi Biden amuondolee mashtaka yanayomkabili mwanzilishi wa tovuti inayofichua nyaraka za siri ya Wikileaks, Julian Assange.

Wiki iliyopita takribani wanasiasa 120, wasanii na waandishi habari waliendesha kampeni na walitoa wito kwa Markel kuzungumzia hatua ya kuachiwa huru Assange katika ziara yake ya Marekani. DVJ imemtaka Merkel na Biden kutozipuuzia sauti za wanaharakati hao, kwani hadi sasa viongozi hao hawajalizungumzia suala hilo.

(AP, DPA, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW