1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Macron wakutana kwa mazungumzo

Yusra Buwayhid
16 Machi 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaelekea Ufaransa kukutana kwa mazungumzo na Rais Emmanuel Macron. Mada kuu wanazotarajiwa kujadili ni kuuimarisha Umoja wa Ulaya na ushirikiano wa nchi zinazotumia sarafu ya euro.

EU Gipfel Macron Merkel
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Kulingana na duru za Ikulu ya Ufaransa Elysee, viongozi hao wawili ambao wamekuwa na uhusiano mzuri tokea Macron alipoingia madarakani mwaka jana, watakutana kwa mazungumzo ya kikazi.

Macron ametoa wito wa kufanya mabadiliko makubwa ya kuuimarisha Umoja wa Ulaya katika wakati ukiwa unakabiliana na changamoto ya siasa kali za mrengo wa kulia zinazoendelea kupata umaarufu. Mapendekezo yake ni pamoja na eneo linalotumia sarafu ya euro kuwa na waziri mmoja wa fedha na bajeti moja.

Katika ukurasa wake wa Twitter Macron alimpongeza Merkel wakati alipochaguliwa tena, na kutoa wito wa kutaka wafanye kazi pamoja kuuimarisha Umoja wa Ulaya.

Ujumbe huo wa Twitter umegusia kile ambacho kinatarajiwa kuwa suala kuu wakati wawili hao watakapokutana: Ajenda ya Macron ya kujenga ushirikiano imara zaidi miongoni mwa nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Hata hivyo haikuwekwa wazi kama viongozi hao wawili watafanikiwa kama walivyopendekeza mwezi Desemba kuwasilisha mapendekezo kamili katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo kuanzia tarehe 23 hadi 24 Machi.

"Kwa hakika hii ndiyo siku ambayo Macron amekuwa akiisubiri," amesema Sebastien Maillard wa Taasisi ya Jacques Delors. "Kunaonekana kuwepo hali ya uharaka," kwa pande zote mbili kuelekea uchaguzi wa Bunge la Ulaya utakaofanyika mwakani, ambao unaweza kuvipa nguvu zaidi vyama ambavyo havipendelea Umoja wa Ulaya, amesema Maillard.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/Y.Herman

Maillard anasema miongoni mwa masuala ambayo Ujerumani na Ufaransa zinaweza kuafikiana ni shinikizo jipya la kukabiliana na mgogoro wa wahamiaji ambao umelitikisa bara la Ulaya, na kodi zaidi kwa makampuni makubwa ya uchumi wa kidijitali. Maillard ameongeza kwa kusema kwamba viongozi hao wawili wanafahamu vyema kuwa mada hiyo itapewa kipaumbele katika uchaguzi ujao wa bunge la Ulaya.

Matokeo ya kushangaza ya vyama vyenye siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa Italia mwezi huu yameongeza hofu ya kwamba vyama vya kisiasa vilivyozoeleka vinaonekana kushindwa kutimiza mahitaji ya wapiga kura.

"Merkel kufanya safari ya haraka kwenda Ufaransa ni ishara ya kwamba anayapa uzito mapendekezo ya Macron," amesema Sabine von Oppeln, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Berlin.

Ziara hiyo iliyopangwa pia ni ishara ya uhusiano wa karibu kati ya Ujerumani na Ufaransa ambao ndio mzizi wa siasa za Umoja wa Ulaya. Aidha Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ameelekea Ufaransa Jumatano iliyopita, masaa machache baada ya kuchukua rasmi wadhifa huo kutoka kwa mtangulizi wake Sigmar Gabriel.

Mwandishi. Yusra Buwayhid/afp/dpa

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW