1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Macron Paris

Zainab Aziz19 Januari 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kukutana kujadili masuala ya kodi na bajeti ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro

Gipfel der EU-Staats- und Regierungschefs | Angela Merkel mit dem französischen Präsidenten Emmanuel Macron
Picha: picture-alliance/AP Photo/dpa/Virginia Mayo

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel watakutana leo Ijumaa mjini Paris, Ufaransa kuangalia mipango ya kukubaliana kuhusu mageuzi katika eneo linalotumia sarafu ya Euro. Viongozi hao pia wanatarajiwa kujadili juu ya masuala ya kodi na bajeti ya ukanda huo wa Euro.

Viongozi hao wanatafuta kuwa na msimamo mmoja katika malengo ya mageuzi. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kutumia muda wa zaidi ya saa  tano pamoja mjini Paris kuonyesha uwepo wa umoja baina ya Ujerumani na Ufaransa huku wakijaribu kukubaliana juu ya mageuzi katika ukanda wa Euro.

Kwenye mkutano wa kilele uliofanyika mjini Brussels mwezi uliopita, viongozi hao wawili walisema wanatumai kuleta mapendekezo  ya pamoja juu ya mageuzi katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro hadi kufikia mwezi Machi. Macron anaweka mkazo juu  ya bajeti ya  kujitegemea pamoja na kuchaguliwa waziri wa fedha wa ukanda  huo.

Majadiliano na Ufaransa yachelewa

Juhudi za Kansela Merkel za kuunda serikali nchjni Ujerumani zimerudisha nyuma majadiliano na Ufaransa. Hata hivyo matumaini ya kuweza kuunda serikali ya mseto na chama cha Social Demokratic SPD yameutia msukumo mpya mjadala juu ya mageuzi katika nchi za ukanda wa sarafu ya Euro.

Ujerumani na Ufaransa ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 50 ya zao la ukanda huo wa Euro ni nchi muhimu katika juhudi zinazolenga kuleta mageuzi katika jumuiya hiyo.

Mwaka huu wa 2018 unazingatiwa kuwa muhimu sana katika kusonga mbele na juhudi za kutekeleza mageuziPicha: Reuters/Y. Herman

Bila ya makubaliano baina ya nchi hizi mbili, malengo yoyote ya kuuboresha umoja wa kifedha na wa kiuchumi ili kuiwezesha  jumuiya hiyo kuikabili migogoro ya siku za usoni malengo hayo hayataweza kutekelezwa.

Wakati ambapo Umoja wa Ulaya unatarajia kufanya uchaguzi mwaka ujao na wakati ambapo Uingereza imo njiani kujiondoa Umoja wa Ulaya (Brexit), mwaka huu wa 2018 unazingatiwa kuwa muhimu sana katika kusonga mbele na juhudi za kutekeleza mageuzi.

Njia ndefu ya kufikia msimamo wa pamoja

Hata hivyo licha ya Kansela Merkel na Rais Macron kukutana na kuzungumza kwa njia ya simu mara kwa mara na licha ya mawaziri wa fedha wa Ujerumani na Ufaransa pia kufanya mazungomzo mjini Paris hapo jana, njia bado ni ndefu ya kuweza kufikia msimamo wa pamoja juu ya masuala ya msingi.

Waziri wa fedha  wa Ufaransa Bruno Le Maire amedokeza baada ya mazungumzo na mwenzake wa Ujerumani Peter Altmaier kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa baada ya mwezi Machi.

Waziri wa Fedha wa Ufaransa Le Maire amesema masuala ya kupewa kipaumbele yanayopaswa kushughulikiwa ni pamoja na kukamilisha umoja  wa benki, umoja wa masoko ya mitaji na uratibishaji wa kodi baina ya Ufaransa na Ujerumani. Bwana Le Maire ameeleza kwamba lengo ni kufanikisha kufikia msimamo wa pamoja juu ya masuala hayo matatu ifikapo kati ya mwezi wa Machi na mwezi Juni mwaka huu wa 2018. 

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE

Mhariri:   Mohammed Abdul-Rahman

    

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW