Merkel : Kura za maoni Ukraine sio halali
10 Mei 2014Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wamesema kura za maoni zilizopangwa kufanyika mashariki mwa Ukraine sio halali na kuionya Urusi juu ya kuchukuliwa hatua zitakazokuwa na taathira mbaya iwapo uchaguzi uliopangwa kufanyika Ukraine Mei 25 utashindwa kufanyika.
Wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwenye mji wa kaskazini mashariki mwa Ujerumani wa Straslund kwamba kile kinachoitwa kura ya maoni zilizopangwa kufanyika katika miji kadhaa mashariki ya Ukraine sio halali na kwamba uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo una umuhimu mkubwa.
Viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa wamemshinikiza Rais Vladimir Putin kufanya jitihada zaidi kutuliza hali ilioko Ukraine na kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wa urais uliopangwa Mei 25 huku Kansela Merkel akisisitiza kwamba Putin lazima achukuwe hatua zaidi ya kuutuliza mzozo wa nchi hiyo.
Merkel amezielezea kile kinachoitwa kura za maoni zilizopangwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi kufanyika Jumapili katika majimbo mawili yenye vurugu mashariki mwa Ukraine kuwa sio halali wakati Hollande akisema kwamba "hazina uzito wowote".
Waasi wanaendelea na mipango ya kupiga kura hiyo licha ya wito wa Putin alioutowa Jumatano wa kutaka kucheleweshwa kwa kura hiyo.
Shinikizo kwa Putin
Merkel amesema yeye na Hollande wamekubaliana kuweka wazi kwamba rais wa Urusi anapaswa kuchukuwa hatua zaidi zenye kuonyesha ishara ya kuutuliza mzozo huo wa Ukraine ili kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wa rais.
Ameongeza kusema kwamba "kumekuwepo na ishara za awali lakini hazina budi kuimarishwa kuhakikisha ujumbe unafika kwa maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine kwamba kila mtu anataka kufanyika kwa uchaguzi mkuu na wa rais ulio huru na wa haki.
"Iwapo jambo hilo halitofanyika , litazidi kuifanya hali ya Ukraine kuwa mbaya" amesema Merkel na kusisitiza kwamba Umoja wa Ulaya itabidi tena hapo kuimarisha zaidi vikwazo vyake dhidi ya Urusi.
Rais Hollande wa Ufaransa ambaye alikutana na Kansela Merkel katika jimbo lake la uchaguzi la Strauslund kaskazini mashariki mwa Ujerumani katika ziara yake ya siku mbili amesema wana uhusiano na Vladimir Putin ambao wanautumia ili kwamba azingatie kile kilioko hatarini katika wiki zinazokuja nchini Ukraine.
Mazungumzo ya kitaifa
Merkel na Hollande katika taarifa yao ya pamoja pia wametowa wito wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa kati ya serikali ya Ukraine na wawakilishi wa majimbo yote ya Ukraine ambapo wamesema yanapaswa kuwashirikisha watu wote wenye kupinga matumizi ya nguvu. Merkel amesema angelipenda kuona mazungumzo hayo yanaanza wiki ijayo.
Taarifa yao hiyo pia imevitaka vikosi vya usalama vya Ukraine kujiepusha na mashambulizi yoyote yale katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Kura ya maoni itakuwa balaa
Rais wa mpito wa Ukraine Oleksander Turchinov ameyaambia majimbo ya mashariki yaliokumbwa na uasi wa wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi kwamba yatakuwa yanakaribisha balaa iwapo watapiga kura ya "ndio" katika kile kinachoitwa kura ya maoni ya kutaka kujitenga na Ukraine.
Turchinov ambaye anaiona kura hiyo iliopangwa kufanyika katika majimbo ya Donets na Luhansk kuwa sio halali amewataka wakaazi wake wakubali kufanya mazungumzo ya majadala juu ya majimbo hayo kupatiwa mamlaka zaidi ya kujiamulia mambo yao. Lakini katika suala la wapiganaji ambao waliyanyakua majengo ya serikali na polisi amesema "magaidi" hawatoshirikishwa katika mazungumzo hayo.
Turchinov amesema kwenye mtandao wake kwamba wanaopigania kujitawala hawafahamu kwamba jambo hilo litamaanisha maangamizi kamili ya uchumi,mipango ya kijamii na maisha kwa jumla kwa sehemu kubwa ya wananchi walioko kwenye majimbo hayo.
Mataifa ya magharibi yanatazamiwa kutangaza vikwazo vipya vya kiuchumi kutokana na hatua anazochukuwa Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa Ukraine.
Umoja wa Ulaya hadi sasa umeweka marufuku ya viza na kuzuwiya mali kwa raia 48 wa Urusi na Ukraine kutokana na hatua ya Urusi kulinyakuwa jimbo la Crimea. Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanasema vikwazo vipya kwa mara ya kwanza vitayalenga makampuni.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ AP/dpa/Reuters
Mhariri:Mtullya abdu.