Merkel kuzuru China Jumapili
4 Julai 2014Kwa taifa hili lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, China inatoa soko muhimu na kubwa, ambako makampuni yanataka teknolojia ya Ujerumani, na mamilioni ya raia waliopata mafanikio wanatamani sana bidhaa za Ujerumani kuanzia magari ya kifahari hadi vifaa vya anasa vya majumbani.
Merkel anatarajiwa kuambatana na ujumbe mzito wa wafanyabiashara wakiwemo watendaji wakuu wa kampuni za Siemens, Volks Wagen, Airbus, Lufthanza na Deutsche Bank.
Maafisa wa serikali hawakuthibisha orodha hiyo lakini walisema wakuu wa mashirika makubwa wanatarajia kusaini makubaliano ya kibiashara katika ukumbi mkubwa wa umma mjini Beijing, ambayo yataimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo.
China ndiyo mshirika namba mbili wa kibiashara wa Ujerumani nje ya Ulaya baada ya Marekani. Ujerumani iliuza bidhaa zenye thamani ya euro bilioni 67 nchini China mwaka uliyopita, wakati bidhaa zilizoingizwa kutoka China zilikuwa na thamani ya euro bilioni 73.
Udumishaji kasi ya makaribiano
Mkurugenzi wa utafiti katika baraza la uhusiano wa nje la Umoja wa Ulaya Hans Kundnan, alisema mauzo ya Ujerumani nchini China yemeongezeka kwa kiasi kikubwa hasa wakati wa mgogoro wa kiuchumi wa dunia, baada ya kuanguka kwa baadhi ya masoko yake barani Ulaya.
Alisema hivi sana uhusiana wa kutegemeana kati ya nchi hizo mbili, ambapo Ujerumani inahitaji soko la bidhaa zake, wakati China inahitaji Teknolojia ya kisasa kutoka Ujerumani.
Hakuna kiongozi wa Umoja wa Ulaya aliekutana mara nyingi na viongozi wa China kama Kansela Angela Merkel ambaye alikutana na rais Xi Jinping mwezi Machi na pia wajumbe wa serikali mbili wanatarajiwa kukutana tena kwa ajili ya mashauriano mjini Berlin mwezi Oktoba.
Mtaalamu kutoka taasisi ya masuala ya China ya Mercator ya mjini Berlin, Sebastian Heilmann anasema ziara hizi zinalenga kuendeleza makaribiano baina ya mataifa hayo mawili.
"Ziara hizi zinalenga kudumisha kasi ya mahusiano kati ya Ujerumani na China, kuelekea mkutano wa mashauriano mwezi Oktoba ambapo mikataba kadhaa ya teknolojia, elimu na utamaduni itasainiwa," alisema Heilmann.
"Hivyo unahitaji msaada kiongozi wa juu kwa sababu hivi haviwezi kujadiliwa kwa ngazi ya chini, hivyo kwa maoni yangu naona ni moja ya sababu zinazomfanya Kansela kusafiri kwenda China."
Wakati wa ziara zake za nyuma, Merkel ameonyesha kupendezwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi wa China. Amekuwa akitoa hoja kwamba bara la Ulaya lilikumbwa na migogoro linahitaji kubadilika na kufanya mageuzi ikiwa linataka kunufaika na soko la kimataifa wakati ambapo mataifa yenye wakaazi wengi kama China yakizidi kuendelea.
Masuala nyeti kugubika mikutano
Ziara ya Merkel itaanzia Chegndu siku ya Jumapili, mji mkuu wa jimbo la Sichuan, ambalo kwa wakaazi wake milion 80 lina idadi ya wakaazi karibu sawa na Ujerumani.
Katika mji huo wa wakaazi milioni 14, ambako makampuni 160 ya Kijerumani yanaendesha shughuli zake, atatembelea kiwanda cha magari cha Volks Wagen, na anatarajiwa pia kutembelea kituo kinachowasaidia watoto wa wafanyakazi wahamiaji wa ndani.
Katika mkutano wa pamoja wa biashara mjini Beijing, Ujerumani inatarajiwa kuzungumzia msuala yanayozua mgogoro kama vile upatikanaji wa haki ya masoko kwa makampuni ya kigeni na kuheshimu haki za hataza.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe/DW
Mhariri: Josephat Nyiro Charo