1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Maambukizi mapya ya COVID-19 yanapungua Ujerumani

Sylvia Mwehozi
5 Februari 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kwamba kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya corona kunatoa sababu ya kuwa na matumaini mazuri lakini akaonya kuwa wakati bado ni mgumu

Deutschland | Bundeskanzlerin Merkel im Interview bei ntv und RTL
Picha: Sandra Steins/REUTERS

Kansela Merkel amesema Ujerumani imepita kwenye nyakati ngumu za wimbi la pili la maambukizi wakati visa vya maambukizi mapya vikipungua. Merkel ameyasema hayo katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Ujerumani cha RTL akiongeza kuwa idadi ya watu wanaopatiwa chanjo ya virusi hivyo pia imeongezeka, ingawa amekiri kwamba Ujerumani bado haijafikia malengo yake.

Kansela huyo hata hivyo ametoa tahadhari juu ya kitisho kinacholetwa na aina mpya ya virusi vinavyojibadili na hivyo kuhimiza umma kuelewa haja ya kuendelea na hatua za kufungwa shughuli za umma.

"Nilisema mwanzoni mwa msimu wa baridi kuwa huu utakuwa wakati mgumu kwetu na ndicho kilichotokea. Nyakati mbaya za wimbi la pili zimepita, tunapaswa kuvumilia kidogo kwa muda na chanjo zitazidi kutolewa. Mzigo utapungua hospitalini na wazee hawataumwa tena. Ninayo matumaini lakini ni wakati mgumu sana, " amesema Merkel.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex Picha: Benoit Tessier/POOL/AFP

Nayo serikali ya Ufaransa imesema kwamba haitoanzisha vizuizi vipya dhidi ya COVID, wakati nako idadi ya maambukizi mapya nayo ikionekana kupungua na utoaji chanjo ukiongezeka. Waziri mkuu Jean Castex, amewaeleza waandishi wa habari kwamba kiwango cha vifo vya Ufaransa wakati wote wa wimbi la pili kilikuwa cha chini na hiyo imetokana na kuimarishwa kwa vizuizi mwezi uliopita ikiwemo marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni. Hata hivyo waziri huyo mkuu amedai kuwa "huu sio muda" wa kuondoa vizuizi hivyo ambavyo vinajumuisha kufungwa kwa maduka na migahawa sambamba na vizuizi vya mipakani.

Na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametoa ripoti hii leo inayosema janga la COVID-19 limeongeza kitisho kutoka kwa makundi yenye itikadi kali ikiwemo kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na Al Qaeda katika maeneo yaliyo na mizozo ikiwa ni pamoja na Afghanistan, Syria na Iraq lakini tishio limebaki chini kulinganisha na maeneo ambayo hayana mizozo licha ya mkururo wa mashambulizi barani Ulaya.

Jopo la wataalamu lilisema katika ripoti iliyosambazwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kitisho zaidi kimeonekana katika nusu ya mwisho ya mwaka 2020 kwasababu janga hilo lilizuia utekelezaji wa sheria na kanuni kulinganisha na magaidi ambao waliweza kukusanyika kwa wepesi licha ya vizuizi vya COVID-19.

Wakati huohuo shirika la afya ulimwenguni WHO kanda ya Ulaya, limesema kwamba Ulaya na makampuni ya dawa yanapaswa kufanya kazi kwa pamoja katika kuongeza kasi ya utoaji chanjo ya covid-19. Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge ameelezea wasiwasi kuhusu ufanisi wa chanjo kwenye aina mpya ya virusi. Amesema "makampuni shindani ya dawa ni lazima yaunganishe nguvu kuongeza uwezo wa kutengeneza chanjo" akiongeza kuwa hicho ndicho kinachohitajika. Ni  asilimia 2.5 ya watu waliopatiwa dozi ya kwanza ya chanjo ya covid katika nchi za Umoja wa Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW