Merkel, Macron waazimia kuimarisha ushirikiano
16 Mei 2017Ziara ya Rais Emmanuel Macron mjini Berlin jana jioni ilikuwa ya kwanza kwake kama rais wa Ufaransa nje ya nchi, baada ya kukabidhiwa rasmi madaraka juzi Jumapili. Alilakiwa na umati wa watu waliokusanyika karibu na ofisi ya Kansela Angela Merkel, baadhi wakipeperusha bendera ya Umoja wa Ulaya. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Merkel na Macron waliojawa na tabasamu, walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi zao kwa manufaa ya Ulaya nzima. Kansela Merkel alisema anaunga mkono Ufaransa yenye nguvu.
''Kila mmoja wetu anasimamia maslahi ya nchi yake, lakini, kijadi maslahi ya Ujerumani yamefungamana na maslahi ya Ufaransa'', alisema Bi Merkel, na kuongeza kuwa. Ujerumani inaweza kufanikiwa tu, ikiwa mambo yanakwenda vizuri Ulaya, na mambo yatakwenda vizuri Ulaya, ikiwa kuna Ufaransa yenye nguvu.
Msukumo mpya kwa Ulaya
Aidha, Kansela Merkel alieleza kuwa yeye na mgeni wake wamekubaliana juu ya mipango kadhaa ya kuupa msukumo mpya uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani, ukiwemo wa mikutano ya mawaziri mwezi Julai baada ya Ufaransa kukamilisha uchaguzi wa bunge.
Viongozi hao wawili hali kadhalika walizungumzia utayarifu wao wa kukubali mabadiliko katika muundo wa Umoja wa Ulaya, kwa madhumuni ya kuufanya umoja huo kuwa wenye ufanisi zaidi. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema yeye hataogopa kuyaleta mezani masuala ambayo siku za nyuma yalikuwa yakinyamaziwa.
Alisema, ''Aghalabu, suala la mabadiliko katika mkataba wa Ulaya limekuwa mwiko nchini Ufaransa. Kwangu haitakuwa hivyo. Matarajio yangu ni kwamba mwelekeo wa pamoja wa Ulaya uwe wa kurejesha ufanisi katika kanda inayotumia sarafu ya yuro, na katika Umoja wa Ulaya. Na ikiwa mchakato huo utahitaji mabadiliko ya kitaasisi, sisi tuko tayari''.
Hofu kuhusu sera ya deni la pamoja
Rais Emmanuel Macron pia alitumia mkutano wa jana kutuliza hofu za wanasiasa wa nchini Ujerumani, kuhusu pendekezo lake la awali la kuwepo bajeti ya pamoja kwa nchi 19 zinazotumia sarafu ya yuro, kwa madhumuni ya kushughulikia vyema zaidi mzozo wa kifedha. Baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani walilichukulia pendekezo hilo kama njia ya kuwatwisha mzigo zaidi walipa kodi wa Ujerumani, mnamo wakati uchaguzi muhimu ukikaribia.
Macron alifafanua kuwa pendekezo lake hilo halilengi kuugawa mzigo wa madeni ya siku za nyuma miongoni mwa wanachama wa kanda ya sarafu ya yuro, akisema badala yake anataka mpango wa pamoja wa siku za usoni katika masuala ya uwekezaji.
Mkutano kati ya viongozi hao wa nchi mbili ambazo zinachukuliwa kama mihimili ya Umoja wa Ulaya, umefanyika wakati umoja huo ukikabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo kujiondoa kwa Uingereza katika mchakato ambao unajulikana kama Brexit, na kukua kwa hisia za kuutilia mashaka umoja huo miongoni mwa raia wa nchi zinazouunda.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe, dw
Mhariri: Iddi Ssessanga