Merkel mgombea rasmi wa CDU na CSU
3 Aprili 2017Chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democrats CDU na washirika wake wa jimbo la Bavaria chama cha Christian Social Union CSU, vimeamua katika mkutano wao wa pamoja mjini Munich kumuunga mkono haraka akiwa kama mgombea wao kwa tikiti ya vyama hivyo katika uchaguzi wa mwezi Septemba ili kusaidia kuzuwia ongezeko la uungwaji mkono kwa chama cha Social Democratic SPD.
Ongezeko la haraka la uungwaji mkono kwa chama cha upinzani cha SPD linakuja baada ya chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto kuishangaza medani ya kisiasa katika taifa hilo kwa kumteua spika wa zamani wa bunge la Ulaya Martin Schulz kuongoza kampeni zake za uchaguzi.
Wakati Schulz ni mtu maarufu katika medani ya siasa barani Ulaya, hafahamiki sana ndani ya Ujerumani, na kusababisha wadadisi wa masuala ya siasa kudokeza kwamba nafasi yake kama mtu asiyefahamika imeongeza mvuto wake.
Chama cha kansela Merkel cha CDU kilimuunga mkono kama mgombea wake wa ukansela katika mkutano wa chama hicho Desemba mwaka jana, lakini chama cha CSU kilikuwa hakijatangaza rasmi uungaji wake mkono hadi katika mkutano huo leo mjini Munich.
"Tunatofautiana katika suala la ukomo wa wahamiaji. Tumeeleza kuhusiana na upinzani huu kwamba tunaheshimu upinzani, lakini pia hatujazuwia upinzani. Nafikiri hili pia ni sahihi na halitafanikiwa."
Washirika wamaliza tofauti zao
Mahusiano baina ya washirika hao wawili hayajakuwa ya utulivu. Kiongozi wa chama cha CSU na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer aliongoza wimbi la ukosoaji kuhusiana na jinsi Merkel alivyoshughulikia mzozo wa wakimbizi baada ya kufungua mipaka ya Ujerumani mwezi Septemba 2015 kuwaruhusu mamia kwa maelfu ya wakimbizi na waombaji hifadhi pamoja na wahamiaji kuingia katika taifa hilo. Lakini leo alisema.
"Kulikuwa na tofauti lakini wakati wote tuliheshimiana na bila kudharauliana. Na leo imekuwa wazi . Tunaingia katika uchaguzi pamoja."
Tangu wakati huo, Merkel mwenye umri wa miaka 62, amerudia mara kwa mara kupuuzia madai ya Seehofer kwamba aweke ukomo kwa idadi ya wakimbizi wanaoingia, na hali hiyo ikasababisha mgawanyiko baina ya CDU na CSU.
Wachunguzi wa maoni ya wapiga kura wamesema hali ya wasi wasi kati ya CDU na CSU kuhusiana na msimamo wa Merkel kwa wakimbizi umechangia kuporomoka kwa kiwango cha juu kwa uungwaji mkono wa vyama vyote hivyo. Suala la uhamiaji linaonekana litaendelea kuleta mgawanyiko ambapo CDU na CSU pia vitapata changamoto kubwa kutokana na kupanda kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, cha Alternative for Germany AfD.
Mchakato wa kuelekea uchaguzi wa mwezi Septemba utaongozana na chaguzi kadhaa za majimbo, ikiwa ni pamoja na jimbo kubwa kabisa nchini Ujerumani la Nort-Rhine Westfalia mwezi Mei. Chaguzi kadhaa zimeonesha ongezeko la uungwaji mkono kwa Schulz mwenye umri wa miaka 61 tangu alipoteuliwa kuwa mgombea wa chama cha SPD katika wadhifa wa ukansela, Jumanne iliyopita pamoja na chama chenyewe.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Gakuba Daniel