Merkel: Mkutano wa G20 kuimarisha ushirikiano
6 Julai 2017Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 unapaswa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Merkel ameyasema hayo leo siku moja kabla ya kuanza mkutano huo hapo kesho mjini Hamburg, katika mkutano wa pamoja na Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong na waandishi habari, na kwamba Ujerumani bado inajizatiti katika kuutekeleza mkataba muhimu wa mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema nchi hizo zimeungana pamoja na nia yao ni kuimarisha uhusiano wa kimataifa katika mkutano wa G20, na wanahitaji kuwa na jamii iliyo wazi, hasa katika masuala ya kibiashara. Merkel pia ameishukuru Singapore kwa mchango wake pindi linapokuja suala la matatizo ya kikanda.
''Kwa ujumla nataka kuishukuru Singapore kwa kutoa mchango wake yanapotokea matatizo ya kikanda, kwa mfano masuala yanayohusiana na Bahari ya kusini mwa China. Tuna imani kuwa nia yetu ni kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili,'' alisema Merkel.
Aidha, Kansela Merkel amesema nchi zote mbili pia zinaunga mkono utekelezwaji wa Mkataba wa mazingira wa Paris, mkataba mkubwa wa kimataifa ambao Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa nchi yake inajiondoa. Merkel amesema tangu Marekani itangaze kujiondoa, basi wasitarajie kuwa mazungumzo ya Hamburg yatakuwa rahisi.
Singapore na Ujerumani zimejizatiti
Kwa upande wake Lee amesema Singapore na Ujerumani zote zimedhamiria kutumia mfumo wa biashara wa soko la wazi la kimataifa, na kwamba anatarajia makubaliano ya biashara huria kati ya Singapore na Umoja wa Ulaya yatafikiwa hivi karibuni, kwani yatasaidia kuzileta karibu zaidi nchi za Kusini Mashariki mwa Asia pamoja na Ulaya.
''Sote tumedhamiria kabisa kuwepo kwa mfumo wa biashara wa soko la wazi la kimataifa, utawala wa sheria pamoja na maendeleo endelevu,'' alisisitiza Lee.
Mkutano wa siku mbili wa G20 pia utaangazia ushirikiano na Afrika. Mpango na Afrika una lengo la kuwavutia zaidi wawekezaji wa umma na wale binafsi katika miradi kadhaa kwenye bara hilo, lakini haitochukua nafasi ya misaada ya maendeleo.
Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 kuhusu Maendeleo Endelevu pia itajadiliwa katika mkutano huo, ambao utahudhuriwa pia na Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Urusi Vladmir Putin na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Wakati huo huo, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Brigitte Zypries amesema leo kuwa makubaliano kuhusu biashara huria yaliyofikiwa kati ya Japan na Umoja wa Ulaya yanatoa ishara muhimu sana dhidi ya sera za kujilinda kibiashara kabla ya mkutano wa G20.
Makubaliano hayo yamesainiwa mbele ya Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, Reuters, http://bit.ly/2sP5QGY
Mhariri: Iddi Ssessanga