Merkel: Mwanamke aliyefanikiwa katika siasa
8 Machi 2012Angela Merkel alizaliwa tarehe 17.7.1954. Baba yake alikuwa mchungaji na mama yake mwalimu na walikuwa wakiishi katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki. Merkel alisomea Fizikia katika chuo kikuu cha Leipzig ambapo alihitimu masomo yake kwa alama nzuri sana. Akiwa bado mwanafunzi, Merkel aliolewa na rafiki yake wa kiume aitwaye Ulrich Merkel, aliyekuwa akisoma naye chuoni. Lakini ndoa hiyo haikudumu na hivyo Angela Merkel aliachana na mumewe lakini aliendelea kulitumia jina lake la ukoo.
Merkel alichelewa kuingia katika ulimwengu wa siasa. Akiwa na umri wa miaka 35, alichaguliwa kuwa naibu msemaji wa Lothar de Maiziere, amabye alikuwa waziri mkuu wa mwisho wa iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki. Uteuzi huo ulifanyika muda mchache baada ya Merkel kujiunga na chama cha Christian Democratic Union (CDU). Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa mbunge na mwaka huo huo Helmut Kohl aliyekuwa Kansela wa Ujerumani wakati huo, alimteua kuwa waziri wa wanawake na vijana. Wanasiasa wengi wa wakati huo walidai kwamba Merkel alichaguliwa tu kwa sababu alikuwa mwanamke mwenye umri mdogo kutoka katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki.
Kupanda cheo kisiasa
Mwaka 1994, Kansela Helmut Kohl alimpa Merkel wadhifa wa kuwa waziri wa mazingira na usalama wa vinu vya nyuklia. Cheo hiki kiliendana na Merkel, kwani ana shahada ya uzamivu katika somo la Fizikia. Merkel alionyesha kuwa mtu anayeweza kusikiliza wengine na kuwa na uwezo mkubwa wa kuwasiliana na watu wengine. Wakati mwingine wanasiasa wenzake wamesema kwamba Merkel anachukua muda mrefu sana kufanya maamuzi.
Angela Merkel aliendelea kupanda cheo kisiasa. Mwaka 1998 alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha CDU baada ya Helmut Kohl kushindwa katika uchaguzi wa ukansela. Na mwaka 2000, Merkel aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa chama chake. Baada ya muda, mwanasiasa huyo alikuwa tegemeo la chama cha CDU. Licha ya kwamba alikuwa amezungukwa na wapinzani, alifanikiwa kuwa mgombea wa ukansela katika uchaguzi wa mwaka 2005. Kwa kuwa chama chake hakikupata kura za kutosha ilibidi kiunde serikali ya mseto na chama cha Social Democratic Party (SPD), lakini Merkel ndiye aliyekuwa Kansela.
Kansela kwa miaka saba sasa
Mwanasiasa huyo aanaeleza kuhusu kile anachokifurahia katika madaraka aliyo nayo: "Kuweza kupanga, kuandaa maamuzi, kusikiliza mawazo ya watu mbalimbali na mwishoni kwa kiasi fulani, kutoa mwongozo wa njia tunayopaswa kuifuata," anaeleza Kensela Merkel. "Wapinzani wanaweza kutoa mawazo mengi, lakini hawana wingi wa kura wa kuweza kupitisha mawazo hayo. Lakini nikiwa kama Kansela, ninaweza kutimiza mambo mengi ambayo ninatamani yafanyike."
Mwanamke huyo mwenye nguvu kubwa kisiasa amekuwa mwenyekiti wa chama chake kwa miaka 12 na kansela kwa miaka 7 sasa. Kuanzia 2008, Merkel amekuwa na kazi kubwa ya kudhibiti migogoro katika siasa za kimataifa, kama vile katika suala la kufilisika kwa nchi ya Ugiriki.
Mwandishi: Wagener, Volker/Dick,Wolfgang
Tafsiri: Shoo, Elizabeth
Mhariri: Josephat Charo