1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Li watetea makubaliano na Iran

Sekione Kitojo
24 Mei 2018

Kansela wa Ujerumani  Angela Merkel na waziri mkuu  wa China Li Keqiang wametetea makubaliano ya kinyuklia na Iran, wakati Li  akisema kusitisha makubaliano hayo kutaleta utata katika majadiliano na Korea kaskazini.

Merkel in China
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Merkel   na  Li  walionesha  msimamo  wa  pamoja  kuelekea  Iran pamoja  na  biashara  huru, masuala  mawili  ambayo  yameshuhudia uingiliaji  kati  wa  Marekani  ambapo  rais  Donald Trump  alichukua hatua  hiyo. Hayo  yalijadiliwa  katika  mkutano  wao  katika  ziara ya  kansela  Merkel  mjini  Beijing.

waziri mkuu wa China Li Keqiang (kushoto) akizungumza na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Li  alionya  kwamba  kusitisha makubaliano  hayo  na  Iran, hakutaiathiri  tu  Iran,  lakini  pia kutakuwa  na  athari  hasi  katika  uwezo  wa  kutatua  masuala mengine  mazito  kupitia  majadiliano  ya  amani.

Hakuitaja  Korea  kaskazini  kwa  jina , lakini  wachambuzi wameonya  kwamba  kujitoa  kwa  Trump  kutoka  katika makubaliano  hayo  na  Iran  kunachafua  uaminifu  wa  Marekani kabla  ya  mkutano  uliopangwa  kufanyika  katika  ya  kiongozi  wa Korea  kaskazini  Kim Jong Un  na  Trump  mwezi  ujao.

Kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel  pia  alieleza  wasi  wasi wake  juu  ya  athari  za  kiuchumi  kwa  Ulaya  kutokana  na  hatua hiyo  ya  Trump  kujitoa  kutoka  katika  makubaliano  na  Iran.

Uamuzi  wa  Trump  kurejesha  vikwazo  dhidi  ya  Iran , licha  ya maombi  kutoka  kwa  washirika  kuendelea  na  makubaliano  hayo, kunaweza  kuathiri  makampuni  ya  ulaya  ambayo  yanafanya biashara   nchini  Iran  tangu  yaliposainiwa  makubaliano  hayo mwaka  2015.

Kansela Merkel akisimama karibu na treni yendayo kasi iliyotengenezwa na kampuni ya Ujerumani nchini China.Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb/epa/R. Vennenbernd

Makampuni  ya  Ulaya 

Iwapo  makampuni  ya  Ulaya  yatajitoa  ama  kupunguza  operesheni zao  nchini  Iran  kwa  kuhofia  vikwazo  vya  marekani , hali  hiyo italeta  fursa  kwa  makampuni  kutoka  mataifa  mengine  kuingia nchini  Iran  na  kufanyabiashara ," Merkel  alisema.

 

kuhusiana  na  biashara  , Merkel  alikaribisha  hatua  ya  China  ya kupunguza  ushuru  kwa  magari  yanayoingia  nchini  humo na kuruhusu  makampuni  ya magari  ya  kigeni  kumiliki  hisa  kubwa katika  miradi ya  pamoja  na  washirika  wao  wa  China.

Kansela  amezungumzia  pia  madai  ya  Ujerumani  kwa  China  ya kupunguza  vizuwizi  katika  uwekezaji  wa  nje , akisema  nchi  hizo mbili  zitatia  saini  makubaliano  ya  kuwezesha  kila  nchi  kupata fursa  ya  kuingia  katika  soko  la  mwenzake  kwa  upande  wa magari.

Waziri mkuu wa China Li KeqiangPicha: picture-alliance/Newscom/S. Shaver

 

"China  na  Ujerumani  zimo  katika  njia  ya  kuhimiza  mahusiano  na mataifa  mengine  pamoja  na  kuimarisha  biashara  huru," alisema Merkel , ambaye  aliongozana  na  ujumbe  wa  viongozi  wa makampuni 18  kutoka  Ujerumani.

Li alidokeza  kwamba   makubaliano  ya  uwekezaji  kati  ya  China na  Umoja  wa  Ulaya, ambayo  yamekuwa  yakifanyiwa  kazi  kwa muda  mrefu, huenda  yakatiwa  saini  wakati  wa  mkutano  wa pande  hizo  mbili  wa  kila  mwaka  mwezi  Julai mjini  Beijing.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusuf , Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW