1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Macron wagusia kuchelewa kwa Brexit

Sylvia Mwehozi
27 Februari 2019

Kansela Angela Merkel amekutana na rais Emmanuel Macron mjini Paris katika mazungumzo yaliyotuama zaidi kwenye suala la Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, uhusiano na Marekani pamoja na masuala mengine ya Ulaya. 

Frankreich, Paris: Staatsbesuch Angela Merkel trifft Emmanuel Macron
Picha: Reuters/G. Fuentes

Mkutano huo unakuja siku moja baada ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kusema kwamba bunge litapata fursa ya kupiga kura kuchelewesha tarehe ya mwisho ya nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya ambayo ni Machi 29. Ucheleweshwaji huo utahitaji kuidhinishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Kwenye mkutano wa pamoja na rais Macron, Kansela Merkel amesema ikiwa Uingereza inahitaji muda zaidi wako tayari kukubalia na ombi hilo.

"Tunakaribia tarehe ya mwisho ya Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya ambayo ni mwishoni mwa mwezi ujao. Wote tunakubaliana na mimi nilizungumza hili na Theresa May siku chache zilizopita huko Sharm el-Sheikh kwamba makubaliano ya kujiondoa ni halali. Ikiwa Uingereza inahitaji muda zaidi, hatutopinga bali tunatafuta suluhisho la pamoja, suluhisho la Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya".

Naye Rais Macron amegusia kwamba kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kurefusha kipindi cha mazungumzo kuhusu kipengele nambari 50 cha Uingereza kujiondoa muungano huo kama itathibitishwa na Uingereza yenyewe na pia kama kuna malengo ya wazi.

Merkel akizungumza na waandishi wa habari Picha: Reuters/G. Fuentes

Aidha anasema "muda umefika" kwa viongozi wa Uingereza kuamua jinsi gani nchi hiyo itajiondoa Umoja wa Ulaya, mnamo wakati kukiwa na dalili kwamba London inaweza kuchelewa kuondoka hadi baada ya Machi 29.

"Tutaunga mkono ombi la kurefusha muda kama litakuwa ndio chaguo jipya la Uingereza", alisema Macron katika mkutano wa pamoja na Kansela Merkel. "Kama alivyowahi kusema Michel Barnier kwamba hatuhitaji muda zaidi bali wengi wetu tunahitaji maamuzi".

Merkel na Macron pia wamegusia ushirikiano wa ulinzi kwa mujibu wa ofisi ya rais Macron.

Suala la kuhusu sera za viwanda pia ni mada iliyogusiwa ambapo nchi zote mbili zinahimiza mabadiliko ya sheria shindani za Umoja wa Ulaya. Pia zinataka uanzishwaji wa viwanda vikubwa vya Ulaya ambavyo wanasema vitaleta ushindani na vile vya kichina na Marekani.

Viongozi hao mnamo mwezi Janauari walitia saini mkataba wa ushirikiano mpya baina ya mataifa hayo mawili. Waliahidi kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya sera za kigeni, kupambana na uhalifu pamoja na ugaidi sambamba na maendeleo ya kimataifa na utafiti.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters/AP

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW