Merkel na mkakati wa jeshi nchini Afghanistan
23 Aprili 2010Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametetea uwepo wa vikosi vya jeshi la nchi hiyo nchini Afghanistan. Amesema kuondolewa mapema kwa wanajeshi hao nchini humo itakuwa ni kwenda mbali mno zaidi kuliko hata mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001.
Akizungumza bungeni jana, Bibi Merkel alisema usalama wa Ujerumani unategemea ushindi dhidi ya wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan. Aidha, Kansela huyo aliwataka wananchi wa Ujerumani kuwaunga mkono wanajeshi walioko nchini Afghanistan. Ameongeza kusema kuwa hatua ya kuwepo wanajeshi hao nchini humo inafuata sheria ya kimataifa na katiba ya Ujerumani.
Vyama vya upinzani vya Social Democtrats na kijani vimeonyesha wasi wasi wao iwapo mikakati ya sasa ya Afghanistan iko imara kupambana na wapiganaji wa Taliban na al-Qaeda. Nacho chama cha mrengo wa shoto kimetaka kuondolewa haraka kwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan.