1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Putin kujadili Afghanistan na masuala mengine

20 Agosti 2021

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Vladmir Putin wa Urusi wanafanya mazungumzo mjini Moscow wakati mgogoro ukiendelea kufukuta Afghanistan,

Angela Merkel und Vladimir Putin
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Masuala mengine yanayotarajiwa kuibuka katika mkutano huo ni mradi wa bomba la gesi kati ya Urusi na Ujerumani unaopingwa na Marekani, ukandamizaji wa upinzani nchini Belarus na madai kuwa serikali ya Belarus inawalazimisha wahamiaji kuingia Latvia, Lithuania na Poland kwa lengo la kuudhoofisha Umoja wa Ulaya.

Ziara ya Merkel mjini Moscow inakuja wakati Kansela huyo akikaribia mwisho wa uongozi wake wa karibu miaka 16 wa Ujerumani. Yeye na Putin, ambaye amehudumu kama rais wa Urusi au waziri mkuu tangu 2000, walimudu kuweka mawasiliano ya mara kwa mara kwa miaka mingi licha ya tofauti zao nyingi za kisiasa.

Hata hivyo, uhusiano wa kibinafsi kati ya viongozi hao umezorota tangu 2014, wakati Urusi ilipochukua kwa nguvu Rasi ya Crimea nchini Urusi na kuwaunga mkono waasi wanaopigania kujitenga mashariki mwa Ukraine, na pia vitendo vingine vya kimabavu vya Moscow.

Wachambuzi hata hivyo wana mashaka kama mkutano wa Merkel na Putin utaimarisha mahusiano ya Ujerumani na Urusi.

Soma pia:Merkel, Putin wahimiza kutulizwa mivutano mashariki Ukraine

Mchambuzi wa kisiasa kutoka Baraza la Ujerumani kuhusu Mahusiano ya Kigeni Stefan Meister anasema Urusi imekuwa utawala wa kimabavu. Na kuzorota kwa mahusiano kati ya nchi hizo kunadhihirishwa katika kuharibika kwa uhusiano wa kibinafsi wa viongozi hao wa muda mrefu. "Kimsingi, mahusiano kati ya Ujerumani na Urusi yamezorota kabisa. Yanaharibika kila mwaka. Merkel hatoweza kushawishi lolote katika mazungumzo hayo. Lakini bila shaka atajadili masuala haya, Nord Stream 2, Donbas, masuala ya usalama Afghanistan. Na huo ndio utakuwa urithi wake."

Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert aliwaambia waandishi wa habari wiki hii mjini Berlin, kuwa mazungumzo ya leo mjini Moscow yatakuzwa kuhusu maswali makubwa ya kimataifa yanayostahili majibu.

Kansela Merkel ameelekea Urusi katika mkesha wa kumbukumbu ya Navalny kuanza kuugua ghafla wakati akiwa kwenye ndege katika mkoa wa Siberia mnamo Agosti 20, 2020. Kiongozi huyo wa upinzani akahamishiwa Ujerumani kwa matibabu maalum. Madaktari waligundua aliwekewa sumu ya kuuwa mishipa ya fahamu iliyotengenezwa na Wasovieti.

Soma pia: Urusi yajitetea kujiimarisha kijeshi kwenye mpaka na Ukraine

Merkel mwenye umri wa miaka 67, ambaye alikulia katika upande wa Kikomunisti wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na kuzungumza vizuri Kirusi, kila mara anasisitiza kuwa mahusiano na Urusi yanaweza tu kuimarika kupitia mazungumzo. Ziara yake itakuwa moja ya safari za mwisho za kigeni akiwa Kansela kwa vile hatogombea uchaguzi wa Ujerumani mwezi ujao.

Putin mwenye umri wa miaka 68, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 20, ndiye kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi Urusi tangu dikteta wa Kisovieti Josef Stalin.

AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW