Merkel na Putin wajadili mizozo ya Ukraine na Syria
19 Agosti 2018Haya yamefanyika wakati wa mazungumzo mazito nje ya mji wa Berlin ambayo yalimalizika bila kupigwa hatua maalum.
Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari hakuna maendeleo yaliyofikiwa, lakini mkutano huo ulikuwa tu una lengo la "kuangalia vipimo" baada ya mkutano wa Merkel na Putin katika mji wa kitalii ulioko katika bahari nyeusi wa Sochi mwezi Mei.
Mahusiano baina ya nchi hizo mbili yamedhoofika tangu pale Urusi ilipolinyakua kwa nguvu jimbo la Crimea la Ukraine mwaka 2014.
Viongozi hao wawili wote wanauangalia mradi wa bomba la gesi unaojulikana kama Nord Stream 2, kuwa ni mradi wa kibiashara zaidi, licha ya mashambulio ya mara kwa mara kutoka Marekani ,na serikali za Ukraine, Peskov alisema.
Merkel alisisitiza matarajio yake
"Hii ndio sababu ni muhimu kuchukua hatua dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ambayo si ya ushindani na kinyume na sheria kutoka katika nchi ya tatu ili kuweza kukamilisha mradi huu hatimaye," aliwaambia waandishi habari muda mfupi kabla ya Putin kurejea nyumbani nchini Urusi. Haikufahamika mara moja ni "hatua" gani zinaweza kuhusika.
Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Merkel alisisitiza matarajio yake kwamba Ukraine inapaswa kuendelea kuwa na jukumu kama nchi inayopitia gesi katika Ulaya, na kukaribisha mwanzo wa majadiliano miongoni mwa Umoja wa Ulaya, Ukraine na Urusi kuhusiana na suala hilo.
Putin, akizungumza katika kasri la serikali ya Ujerumani la Meseburg, alisema hatua kama hizo zinapaswa kueleweka kwa mtazamo wa kibiashara.
"Suala kuu ni kwamba nchi ya Ukraine kama sehemu ya kupitia, ambayo ni ya asili kwetu, inatimiza mahitaji ya kiuchumi" alisema. "Nord Stream 2 ni mradi wa kiuchumi tu."
Marekani inaibinya Ujerumani kusitisha bomba hilo ambalo linasafirisha gesi kutoka Urusi chini ya bahari ya Baltic, ikidai kuwa itaongeza utegemezi wa Ujerumani kwa Urusi kwa ajili ya nishati.
Ukraine inahofia kwamba bomba hilo litaruhusu Urusi kuitenga katika biashara ya kuwa nchi inayopitia gesi, wakati majirani wa Ujerumani upande wa Mashariki mwa Ulaya waan hofu juu ya hatua za Urusi kuziingilia.
Peskov amesema kitisho hicho cha uwezekano wa vikwazo vya Marekani dhidi ya makampuni yanayohusika katika mradi huo hakikujadiliwa katika mkutano wa hapo jana Jumamosi.
Ni muhimu kuepusha mzozo wa kibinadamu Idlib
Akisimama pamoja na Putin kabla ya mazungumzo hayo, Merkel alisema nchi hizo mbili, lakini hususan Urusi kama mwanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa , ina jukumu la kujaribu kutatua mapigano yanayoendelea nchini Ukraine na Syria.
Amesema anapanga pia kuzusha masuala ambayo yanaonekana kuwa vikwazo ya haki za binadamu kwa Putin, na kujadili mahusiano ya pande mbili.
"Nina maoni kwamba masuala yenye utata yanaweza tu kutatuliwa kupitia majadiliano na katika majadiliano," amesema.
Merkel amesema ni muhimu kuepusha mzozo wa kibinadamu katika jimbo la Idlib, Syria pamoja na majimbo ya karibu, na kusema yeye pamoja na Putin tayari wamelijadili suala la mabadiliko ya katiba pamoja na uwezekano wa uchaguzi wakati walipokutana mjini Sochi mwezi Mei mwaka huu.
Putin aewaambia waandishi habari kwamba kila kitu ni lazima kifanyike kuwasaidia wakimbizi wa Syria kurejea katika nchi yao na kwamba Syria inahitaji msaada wa kuijenga upya. Viongozi hao wawili hawakujibu maswali ya waandishi habari.
Kuhusu Ukraine, Merkel alisema ana matumaini kwamba juhudi mpya zinaweza kuchukuliwa mwanzoni mwa mwaka mpya wa masomo kutenganisha majeshi ya Ukraine na yale wanaotaka kujitenga katika maeneo ya mstari wa mbele katika jimbo la Donbass.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Jacob Safari