1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Seehofer waafikiana kuhusu uhamiaji

Josephat Charo
2 Julai 2018

Seehofer amesema muafaka umepatikana katika mzozo uliotishia kuiangusha serikali ya mseto ya Ujerumani inayoongozwa na kansela Angela Merkel.

Deutschland, Berlin: Asylstreit - Merkel nach Fraktionssitzungen
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na waziri wake wa mambo ya ndani, Horst Seehofer, wamekubaliana dakika ya mwisho na kuondosha tofauti zao kuhusiana na mvutano juu ya sera ya uhamiaji. Hatua hiyo inaashiria serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Merkel inabaki kuwa imara, kinyume na hofu iliyokuwepo kwamba ingevunjika.

Kansela Merkel amesema Ujerumani itawazuia wahamiaji waliosajiliwa katika nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya kwenye vituo maalumu, huku ikiwa katika mchakato wa kutafuta njia za kuiwarejesha makwao. Merkel amesifu makubaliano yaliyoafikiwa na washirika wake wa Bavaria ambao walikuwa wametishia kujiondoa kutoka serikali yake ya mseto.

Alisema muafaka kati ya chama cha Christian Social Union, CSU, na Christian Democratic Union, CDU, utasaidia kulinda kanuni ya uhuru wa watu kutembea katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya huku ukiiruhusu Ujerumani kuchukua hatua katika ngazi ya kitaifa kupunguza na kudhibiti idadi ya wakimbizi wanaowasili.

"Tunataka kwa upande mmoja kujenga vituo vya muda vya wahamiaji Ujerumani na kuanzia hapo tuwarejeshe makwao chini ya makubaliano na nchi wanakotokea waomba hifadhi na ambako tayari wamesajiliwa," Merkel aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu.

Mwandishi: Josephat Charo/dpae/afpe/rtre

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW