1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Ni vigumu kusema kwaheri

18 Novemba 2016

Kansela Angela Merkel amemshukuru Rais Barack Obama kwa ushirikiano wao wa miaka mianne. Walikuwa na mengi za kuzungumza mjini Berlin, wakati Donald Trump, mkosoaji wa kila mara wa Merkel anajiandaa kuiongoza Marekani

Deutschland Pressekonferenz vom US-Präsident Obama in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Rais wa Marekani Barack Obama amesema angempigia kura Kansela Angela Merkel kama angekuwa na uwezo na kama angegombea tena uchaguzi mwaka ujao. Akizungumza kazika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari mjini Berlin jana, Obama alimsifu Merkel kama "mshirika bora”.

Merkel alisema ingawa yeye na Obama hawakuelewana mara kwa mara, walishirikiana katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kuulinda usiri katika vita dhidi ya ugaidi na kuhimiza mikataba ya kibiashara.

Obama akikaribishwa Berlin na mwenyeji wake MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

"Ni vigumu kwangu kusema kwaheri Obama". Alisema Merkel, wakati akimshukuru kwa miaka minane ya ushirikiano wa karibu na kirafiki.

Viongozi hao wawili walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika wakati huu wa kutokuwa na uhakika kutokana na ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani. Alipoulizwa na wanahabari kuhusu mahusiano ya usoni kati ya Marekani na Urusi chini ya Trump, Obama alisema.."ili na sisi tuweze kutatua matatizo mengi makubwa kote ulimwenguni, ni kwa maslahi yetu kufanya kazi na Urusi". Lakini aliongeza kuwa anatumai rais ajaye atasimama kidete dhidi ya Rais wa Urusi Vladmir Putin wakati akikiuka maadili na kanuni za kimataifa.

Obama alimwambia Merkel kuwa Ujerumani "inapaswa kujivunia namna inavyoushughulikia mgogoro wa wahamiaji, ambao ni hadithi ya mafanikio makubwa waliyoyaanzisha wajerumani".

Kikao hicho cha wanahabari kilifuatia mkutano baina ya viongozi hao wawili, ambapo kinyume na ziara maarufu za zamani za Obama katika mji huo mkuu wa Ujerumani, rais huyo hakutubia katika mikutano ya umma.

Obama ni kiongozi maarufu kwa WajerumaniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Monsivais

Badala yake alishiriki chakula cha jioni na Merkel siku ya Jumatano, na akahojiwa na televisheni ya umma hapa Ujerumani ARD na jarida la "Spiegel" kabla ya kukaribishwa na Kansela ofisini mwake.

Katika mahojiano hayo, Obama kwa mara nyingine alimsifu Kansela wa Ujerumani akisema ni kiongozi mwenye uadilifu mkubwa na ambaye yuko tayari kupigania maadili hayo katika njia ambayo ni muhimu sana.

Viongozi hao wawili walikua na ugumu kuelezea umuhimu wa mahusiano ya kiuchumi kati ya Marekani na Ujerumani, hasa kitisho kilichopo kwa mkataba wa kibiashara kati ya Marekani na Ulaya – TTIP. Merkel alikiri jana kuwa mazungumzo kuhusu muafaka huo hayawezi kukamilishwa katika wiki zilizosalia katika uongozi wa Obama. Na hata ingawa Trump tayari ameashiria upinzani wake kuhusu makataba huo, Merkel aliongeza kuwa ana uhakika siku moja wataweza kurejea tena katika mazungumzo hayo.

Leo asubuhi, Obama atarejea katika ofisi ya Kansela Merkel kwa mazungumzo na viongozi wengine wa Ulaya: Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi, Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May. Mara hii, mada kuu itakuwa mustakabali wa mkataba wa kibiashara kati ya Marekani na Ulaya:

Mwandishi. Bruce Amani/DW
Mhariri. Daniel Gkuba