1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Putin waujadili mzozo wa mashariki mwa Ukraine

9 Aprili 2021

Rais wa Ukraine amezuru uwanja wa mapambano wakati ambapo kuongezeka kwa mivutano kumezusha hofu ya kurejea tena mapigano ya kiwango kikubwa. Ujerumani, Urusi na Marekani zimetoa wito kwa pande husika kujizuia

Paris Ukraine-Gipfel Merkel Putin
Picha: Reuters/C. Platiau

Maafisa nchini Ukraine na nchi za Magharibi wameelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo la kiviwanda la Ukraine, linalofahamika kama Donbas. Pia wameelezea wasiwasi kuhusu kujikusanya kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine.

Ziara ya jana ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mkoa wa Donbas ilikuja wakati mapigano kati ya jeshi la Ukraine na wanaharakati wanaopigania kujitenga wakiungwa mkono na Urusi yakiongezeka katika wiki za karibuni. Zelensky amewashukuru wanajeshi wake kwa kuilinda nchi "Kwanza kabisa, ziara hii ni muhimu kwa walinzi wetu. Ni muhimu kujua kuwa serikali yao inawaunga mkono. Kuna hali ya kuongezeka machafuko hapa Donbas. Hakika, sote tunaona hilo. Wapiganaji, amiri jeshi mkuu na makamanda wote wanaliona hilo. Tunaona walenga shabaha wanawauwa watu wetu." Amesema Zelensky.

Rais wa Ukraine Zelensky akiwa DonbasPicha: Ukrainian Presidential Press/REUTERS

Katika mazungumzo ya simu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Urusi Vladmir Putin alitaja vitendo vya uchokozi kutoka kwa serikali ya Kyv, ambayo imeamua kuongeza mivutano kwenye ukanda wa udhibiti kati ya vikosi vya Ukraine na wanaharakati wanaotaka kujitenga.

Soma pia: Ukraine yaifungulia kesi ya tisa Urusi kwenye Mahakama ya Ulaya

Merkel alijadili na Putin suala la Urusi kupeleka wanajeshi wake katika eneo la karibu na mashariki mwa Ukraine, na akatoa wito wa kuondolewa vikosi hivyo ili kuupunguza mzozo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki alisema Marekani inaendelea kuwa na wasiwasi kutokana na vitendo vya karibuni vya uchokozi vya Urusi mashariki mwa Ukraine, ikiwemo kuwapeleka wanajehsi kwenye mpaka wa Ukraine.

Zelensky, ambaye ameiomba NATO kuharakisha uwanachama wan chi yake katika muungano huo wa kijeshi kuiunga mkono Ukraine, amesema aliyatembelea maeneo ambako idadi kubwa ya ukiukaji wa mpango wa kuweka chini silaha imetokea.

Mjini Moscow, akizungumza katika jopo la mashauriano na watalaamu wa kisiasa, Dmitry Kozak, mshauri wa Putin anayehudumu kama mpatanishi mkuu wa Urusi katika mazungumzo na Ukraine, alionya Ukraine dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi ili kuyakomboa maeneo ya mashariki, ambako wakaazi wengi walichukua uraia wa Urusi

Mzozo wa muda mrefu mashariki mwa Ukraine yamesababisha vifo vya Zaidi ya watu 13,000 tangu 2014.

AFP
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW