Merkel na Hollande wataka Ulaya kuungana kuhusu wahamiaji
8 Oktoba 2015Merkel ameyasema hayo katika hotuba ya pamoja na Rais wa Ufaransa Francois Hollande hapo jana katika bunge la Umoja wa Ulaya ambapo wametoa wito kwa viongozi wenzao wa Ulaya kuungana ili kuweza kukabiliana kwa kauli moja na matatizo yanayowakibili likiwemo kuimarisha uchumi, kuiwezesha zaidi kanda inayotumia sarafu ya euro,suala la wahamiaji, vita vya Syria,kupambana dhidi ya kitisho kutoka kwa Urusi na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu-IS.
Merkel ametoa wito wa kuwepo utaratibu mpya wa kugawana wahamiaji miongoni mwa nchi zote 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya, mfumo utakaochukua sehemu ya ule uliopo ujulikanao kama mchakato wa Dublin ambao unaeleza kuwa nchi ya kwanza aingiayo mhamiaji ndipo atakapoomba hifadhi. Bi Merkel, amesema chaguo bora kwa Ulaya ni kuushughulikia mzozo wa wakimbizi kwa pamoja.
Umoja wa Ulaya ukishirikiana utakuwa imara zaidi
''Kama tunataka kuyashughulikia masuala haya, ni lazima Umoja wa Ulaya ushirikiane, na kujizuia kurejea katika enzi ambapo kila nchi ilifanya kazi kwa misingi ya kitaifa. Tufanye kazi pamoja.''
Kansela huyo wa Ujerumani amesema kuambatana na mfumo huo wa zamani, Ugiriki na Italia zitazidi kulemewa na mzigo mkubwa wa kuwahifadhi wakimbizi kwani ndiko wanakoingia kupitia bahari ya Mediterania.
Ujerumani kwa hivi sasa ndilo taifa la Ulaya linalopokea wahamiaji wengi zaidi wanaotoroka vita na umaskini, idadi ambayo inatarajiwa kuzidi laki nane, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wahamiaji kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Hapo jana maafisa wa Ujerumani walisema wamewasajili kiasi ya wahamiaji 577,000 katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, thuluthi moja ya watu hao wakidai kutokea Syria.
Katika mahojiano katika kituo cha televisheni cha Ujerumani cha ARD jana jioni, Merkel ameutetea msimamo wake kuhusu kuwapokea maelfu ya wakimbizi nchini humu na kusema anajivunia kuona kile alichokitaja sura ya kirafiki ambayo Ujerumani imeuonyesha ulimwengu.
Palipo na nia pana njia
Hata hivyo amekiri kuwa kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko hilo la wakimbizi itakuwa kibarua kigumu kwa taifa hili, na kuongeza lakini kuwa ana imani kwamba Ujerumani itaweza kumudu.
Hollande kwa apande wake amekiri kuwa Umoja wa Ulaya ulichukuwa muda sana kung'amua kuwa mizozo katika kanda ya Mashariki ya kati na Afrika ingekuwa na athari kwa mipaka yake.
Kiongozi huyo wa Ufaransa pia ametoa onyo kali kuwa mizozo inayoendelea mashariki ya kati huenda ikawa na athari kubwa kiusalama kwa Ulaya hasa iwapo umwagaji damu unaondelea Syria hautakomeshwa.
Hollande ameongeza kusema kile kinachojiri Syria kinaihusu Ulaya na iwapo mapigano kati ya wasunni na washia yataruhusiwa kuendelea, hadhani kama Ulaya itakuwa salama kwani ni vita kamili vitakavyosambaa kwingineko.
Mara ya mwisho viongozi wa Ujerumani na Ufaransa walisimama pamoja kutoa hotuba mbele ya bunge la Ulaya ilikuwa miaka 26 iliyopita wakati Rais wa Ufaransa Francois Mitterrand na Kansela wa Ujerumani Helmut Kohl walipotoa hotuba ya pamoja wiki chache baada ya ukuta wa Berlin kuangushwa mwezi Septemba mwaka 1984.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa
Mhariri:Daniel Gakuba