1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Ujerumani haitopeleka silaha yoyote nchini Uturuki

Sylvia Mwehozi
17 Oktoba 2019

Kansela Angela Merkel amelihutubia bunge la Ujerumani kabla ya kuelekea mjini Brussels kuhudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, huku pia akibainisha kuwa nchi yake haitopeleka silaha Uturuki. 

Bundestag Angela Merkel
Picha: Bundestag Angela Merkel

Kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, Kansela Merkel amesema kwamba licha ya muungano kujiandaa kwa ajili ya Brexitisiyo na makubaliano, lakini watafanya majadiliano hadi dakika ya mwisho, na kwamba hadi sasa wako katika njia sahihi ingawa makubaliano bado hayajafikiwa.

"Kumekuwa na harakati katika siku za hivi karibuni, harakati muhimu. Upande wa Uingereza umeonyesha utayari wa kujadiliana na kubainisha mapendekezo. kwahiyo tuko nia bora kuliko awali, lakini leo lazima nisema wazi kwamba bado hatujafikia lengo," alsema Merkel.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, mjini Toulouse huko Ufaransa, Merkel na rais Emmanuel Macron, walisema kwamba wanatarajia makubaliano kufikiwa katika mkutano unaokuja. Wakati tarehe ya mwisho ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya ikikaribia, matumaini yanazidi kuongezeka kufikia suluhisho la kisiasa, na maelezo kamili ya kisheria yakitatuliwa baadae.

Bunge la Uingereza tayari limeshaikataa mara tatu mikataba tarajiwa. Hata kama mkataba utatolewa wiki hii, hatua katika bunge la Uingereza zinaweza kumaanisha kucheleweshwa tena kwa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya oktoba 31.

Kansela Merkel na rais Emmanuel Macron walipokutana mjini Toulouse UfaransaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Scheiber

Hakuna kupeleka silaha Uturuki

Merkel pia alizungumzia operesheni za kijeshi za Uturuki zinazoendelea kaskazini mwa Syria, akisisitiza kuwa Ujerumani haitopeleka silaha ya aina yoyote nchini Uturuki. "Mara kadhaa katika siku za hivi karibuni nimeihimiza Uturuki ikiwemo mazungumzo binafsi na rais wa Uturuki, kukomesha operesheni za kijeshi dhidi ya jeshi la kikurdi la YPGna nasisistiza tena".

Uturuki ilianzisha operesheni hizo wiki iliyopita ikayalenga majeshi ya Kikurdi yanayoungwa mkono na Marekani, baada ya uamuzi wa Marekani wa kuondoa askari wake katika mpaka.

Uvamizi wa Uturuki nchini Syria na namna Umoja wa Ulaya ulivyolipokea suala hilo ni masuala yatakayotawala pia mazungumzo ya viongozi wa muungano huo mjini Brussels. Umoja wa Ulaya ambao umekuwa na mahusianob ya karibu na Uturuki katika masuala kadhaa kama vile uhamiaji na biashara, imejizuia kuweka vikwazo.

Mada nyingine zilizo kwenye ajenda ya mkutano wa kilele ni pamoja na majadiliano juu ya mfumo wa bajeti ijayo ya muda mrefu ya Umoja wa Ulaya, inayomalizika mwishoni mwa mwaka.

Pia Macedonia ya Kaskazini na Albania zinasubiri kauli kutoka Umoja huo ikiwa zinaweza kuanza mazungumzo ya kujiunga baada ya mawaziri wa Umoja wa Ulaya kushindwa kufikia makubaliano juu ya hatua inayofuata kufuatia upinzani kutoka kwa Ufaransa.

Merkel amesema atazishawishi nchi ambazo bado zina upinzani kuhusu kuanzisha mchakato wa mazungumzo ya nchi hizo mbili kujiunga na umoja wa ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW