1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Uwezekano wa mkataba wa Brexit bado upo

9 Desemba 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametilia mashaka matumaini ya kupatikana kwa mkataba kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza juu ya biashara baada ya Brexit.

Symbolbild Brexit Verhandlungen
Picha: picture-alliance/empics/S. Rousseau

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewaambia wabunge mjini Berlin kuwa hali ya mazungumzo kuhusu biashara baada ya Brexit bado iko vile vile kama awali.

Kansela huyo wa Ujerumani amesisitiza juu ya umuhimu wa kujiandaa na mapema kwa kutofaulu kwa mazungumzo hayo.

Merkel amesema "Bado kuna nafasi ya kufikiwa makubaliano. Sina uhakika iwapo tutajua iwapo mazungumzo hayo yatakuwa yamefaulu kufikia kesho, siwezi kuahidi lolote. Hata hivyo, tumejiandaa kwa uwezekano wa kutopatikana kwa makubaliano iwapo kwa mfano Uingereza itakuwa na masharti ambayo hatuwezi kuyakubali. Jambo la muhimu zaidi ni kuwa soko la Umoja wa Ulaya lazima lilindwe."

Soma zaidi: Uingereza na Umoja wa Ulaya kurejea mezani

Muda wa mpito wa Uingereza kusalia katika Umoja wa Ulaya unakamilika Januari mosi, na hivyo basi kuibua wasiwasi mkubwa kuwa huenda Uingereza ikaondoka kutoka Umoja huo bila ya kufikiwa makubaliano yoyote.

Boris Johnson anatarajiwa kusafiri hadi Brussels kwa mazungumzo ya dakika ya mwisho

Picha: Peter Summers/Getty Images

Viongozi wa Uingereza na Umoja wa Ulaya watakutana kwa hafla ya chakula cha jioni leo Jumatano, mkutano huo ukitajwa kuwa muhimu wa iwapo muafaka utapatikana au la. Kama Kansela Merkel, Uingereza pia inaelezea matumaini yenye tahadhari.

Michael Gove ni waziri nchini Uingereza anayehusika na mchakato wa Brexit: "Kwa kweli, tunataka kupata makubaliano lakini nasisitiza sio kwa gharama yoyote. Natumai kuwa tutaona maendeleo katika mazungumzo haya leo jioni au hata siku kadhaa zijazo. Lakini, sitaki kuwa mtu wa kufanya maamuzi wakati huu. Uamuzi utachukuliwa na Waziri Mkuu na baraza la mawaziri."

Waziri Mkuu Boris Johnson anatarajiwa kusafiri leo Jumatano hadi mjini Brussels ili kufanya mkutano binafsi na Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Miezi kadhaa ya mazungumzo imeshindwa kupata mwafaka, huku masuala matatu muhimu yakikosa kupata suluhu kabisa: Uvuvi, Mfumo wa kutekeleza makubaliano, na suala la forodha.

Uingereza imekuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya kwa miaka 47 lakini bado imesalia ndani ya soko huria la Umoja huo hadi mwisho wa mwaka huu.

Kuafikiwa kwa mkataba wa kibiashara baada ya Brexit kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza kutahakikisha kutokuwa na upendeleo wa kibiashara au ushuru wa ziada unaotozwa bidhaa.

Hata hivyo, kinyume chake ni kuwepo kwa vizuizi vya kibiashara ambavyo vinatajwa kuwa huenda vikawa na athari hasi kwa biashara kwa pande zote mbili.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW