1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Zelensky waujadili mradi wa gesi wa Nord Stream 2

23 Agosti 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametaka kuendelezwa mbele kwa juhudi za mazungumzo ya amani juu ya mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Ukraine | Angela Merkel und Wolodymyr Selenskyj
Kansela Angela Merkel na Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Sergey Dolzhenko/Pool Photo/AP/picture alliance

Merkel ameyasema hayo alipokutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy mjini Kyiv ambapo miongoni mwa mambo mengine, viongozi hao wamejadili juu ya juhudi za amani mashariki mwa Ukraine na mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2 unaopingwa na Ukraine. 

Soma zaidi: Marekani na Ujerumani zafikia muafaka mradi wa bomba la gesi la Urusi

Bi Merkel amesisitiza kujitolea kwa Ujerumani kutoiruhusu Urusi kutumia mradi mpya wa bomba la gesi wa Nord Stream 2 kama silaha wakati alipofanya ziara nchini Ukraine ambayo huenda ikawa yake ya mwisho kama kiongozi wa Ujerumani.

"Tumeweka wazi kwamba, tutashinikiza vikwazo zaidi kutoka Umoja wa Ulaya iwapo madai ya Urusi kutumia mradi huu wa bomba la gesi kama silaha, yatathibitishwa."

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky jana Jumapili, Merkel pia ametilia mkazo kufanyika mkutano kati ya Urusi, Ukraine, Ujerumani na Ufaransa kujadili juu ya mzozo wa mashariki mwa Ukraine, mkutano huo ukiwa wa kwanza tangu mwaka 2019.

Ziara ya Merkel inakuja siku mbili tu baada ya kuitembelea Urusi na kukutana na Rais Vladimir Putin. Kansela huyo hatowania tena wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwezi ujao wa Septemba, na anakaribia kumaliza muda wake wa kuhudumu kama Kansela, wadhifa alioushikilia kwa karibu miaka 16.

Mapigano kati ya vikosi vya Ukraine na waasi wanaoungwa na Urusi yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 14,000 tangu mwaka 2014. Ujerumani na Ufaransa zimejitahidi kuwa wapatanishi juu ya mzozo huo.

Ukraine inaupinga mradi wa Nord Stream 2 ukisema unatumiwa na Urusi kama silaha ya kisiasa

Ujenzi wa mradi wa gesi wa Nord Stream 2Picha: Gascade/eugal.de

Zelensky amesema Ukraine inataka usitishwaji kabisa wa mapigano mashariki mwa Ukraine, kubadilishana wafungwa, kufungua mipaka na kuruhusu ufikiaji wa misaada katika eneo lenye mzozo.

Rais huyo wa Ukraine ameunga mkono wazo hilo la kufanyika mkutano, lakini akayahimiza mataifa ya Magharibi kuishinikiza Urusi ili kufikia maendeleo na suluhu ya kudumu mashariki mwa Ukraine.

Merkel ametanabahisha kuwa baadhi ya maombi yaliyotolewa na Zelensky kama vile kufunguliwa kwa mipaka pamoja na masuala mengine ya kibinadamu bado hayajatekelezwa, na kwamba hali hiyo inaregesha nyuma juhudi za kupatikana kwa maelewano.

Soma zaidi: Zelensky, Macron, Merkel wazungumzia Ukraine mashariki

Kansela huyo wa Ujerumani pia amezungumzia juu ya makubaliano kati ya Marekani na Ujerumani mwezi uliopita ya kuruhusu kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kutoka Urusi hadi Ujerumani bila ya kuwekewa vikwazo vya Marekani kwa mashirika ya Ujerumani.

Ukraine hata hivyo unaupinga vikali mradi huo, na Zelensky ameuita mradi huo kama silaha hatari ya kisiasa ya Urusi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW