Merkel ziarani barani Afrika
14 Julai 2011Leo Merkel, anatazamiwa kukutana na Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan. Nigeria iliyo na idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika, ni mzalishaji mkubwa wa nane wa mafuta kote duniani, lakini nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa umeme.
Wakati wa ziara hiyo nchini Nigeria, Merkel anatazamiwa kuunga mkono ushirikiano katika sekta ya nishati na malighafi, kama alivyofanya wakati wa ziara yake nchini Angola, kituo cha pili cha ziara yake barani Afrika. Alipokuwa Angola, aliunga mkono kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Ujerumani na Angola. Alisema kuwa Ujerumani, ingependa kuwekeza katika sekta za miundo mbinu, viwanda na elimu.
Vile vile Ujerumani ingeweza kushirikiana kutafuta mali ghafi zaidi nchini humo. Merkel alitamka hayo baada ya kukutana na Rais wa Angola José Eduardo dos Santos katika mji mkuu wa Angola, Luanda. Merkel alieanzia ziara yake nchini Kenya, amefuatana na Waziri wa Kilimo, Ilse Aigner na ujumbe wa wafanyabiashara.