1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Saudi Arabia

30 Aprili 2017

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amewasili Saudi Arabia Jumapili (30.04.2017) kwa mazungumzo na viongozi wa taifa hilo yatakayojumuisha vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislam na kuimarisha ushirikiano.

Saudi-Arabien Merkel neben König Salman im Königspalast
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Merkel alipokelewa na Mfalme Salman na viongozi wengine waandamizi wa serikali wakati alipowasili kwenye mji wa magharibi wa Jeddah.Akiwa Saudi Arabia Merkel amesaini makubaliano yenye kutowa fursa ya uwezekano kwa wanajeshi wa Saudi Arabia kupatiwa mafunzo katika kambi za kijeshi za Ujerumani.

Bado haiko wazi matawi gani ya kijeshi watatoka wanajeshi hao wa Saudi Arabia na wangapi wataletwa nchini Ujerumani.Ujerumani na Saudi Arabia pia zimesaini azmio la dhamira kuhusu ushirikiano wa polisi ikiwa ni pamoja na polisi wa kike wa Ujerumani kuwapatia mafunzo walinzi wa kike wa mpakani wa Saudi Arabia na mafunzo katika fani ya usalama wa anga.

Katika ziara yake hiyo ya siku mbili kiongozi huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuwashinikiza viongozi wa Ghuba kuchukuwa hatua zaidi katika kuwapokea wakimbizi na kutowa msaada wa kibinaadamu kuwafariji wakimbizi wanaokimbia mizozo kutoka katika zenye idadi kubwa ya Waislamu.Nchi yake imetowa hifadhi kwa maelfu ya watu kutoka Syria,Iraq na Afghanistan katika siku za hivi karibuni.

Sehemu ya maandalizi ya G20

Kansela Angela Merkel na Mfalme Salman Abdelaziz wa Saudi Arabia wakikaguwa gwaride la kijeshi.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Kama vile wanawake wa mataifa ya magharibi walioitembelea nchi hiyo hivi karibuni Merkel hakufunika kichwa chake wakati alipowasili katika taifa hilo la kifalme la kihifadhina.

Hapo Jumatatu ataelekea Falme za Nchi za Kiarabu ambapo atakuwa na mazungumzo na Mwana mfalme Sheikh Mohammed bin Zayed Al- Nahyan.Hapo Jumanne Markel atakwenda Sochi mji wa kitalii wa Bahari Nyeusi ambako atakutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Mikutano yake mbali mbali ni sehemu ya kujiandaa kwa mkutano wa viongozi wa Kundi la mataifa 20 (G20) yenye maedeleo makubwa ya viwanda na yale yanayoinukia kiuchumi ambao Merkel atauongoza hapo Julai katika mji wa bandari wa Hamburg nchini Ujerumani.Nchi zote mbili Urusi na Saudi Arabia ni nchi wa wanachama wa kundi la G20. Ujerumani hivi sasa inashikilia urais wa kundi la G20.

Suala la Yemen kujadiliwa

Kansela Angela Merkel na Mfalme Salman Abdelaziz wa Saudi Arabia wakiwa katika kasri la mfalme mjini Jeddah.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Akiandamana na ujumbe wa kibiashara wa ngazi ya juu mazungumzo ya Merkel nchini Saudi Arabia pia yatalenga Yemen ambapo Kansela anaunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa usitishaji wa mapigano na suluhisho la kisiasa kwa vita hivyo katili vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati Merkel anatarajiwa kuishinikiza mwenyeji wake Saudia kufanya juhudi zaidi kupunguza vikwazo vya kibiashara miradi ya silaha haimo katika genda ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo mazungumzo yake mjini Jeddah na Mfalme Salman na mwana mrithi wa mfalme Mohammed bin Nayf,Merkel anataka kuzungumzia suala la haki za binaadamu halikadhalika dhima ya wanawake nchini humo ambapo wanawake wanapigwa marufuku kuendesha magari.

Mke wa mwanablogu Raif Badawi ambaye kufungwa kwake na kupigwa viboko hadharani kulishutumiwa kimataifa pia amemtaka Merkel kumuombea msamaha mume wake huyo wakati wa ziara yake nchini Saudi Arabia.

Mwandishi :Mohamed Dahman/dpa/AP

Mhariri: Caro Robi

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW