1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wasema Umoja wa Ulaya utakuwa imara

Admin.WagnerD23 Agosti 2016

Viongozi wa Ujerumani,Ufaransa na Italia wameazimia kuimarisha usalama na kuchukua hatua zaidi ili kuleta nafasi zaidi za ajira kwa watu wao.

Viongozi wa Ujerumani,Ufaransa na Italia wakutana Ventotene
Viongozi wa Ujerumani,Ufaransa na Italia wakutana VentotenePicha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/G. Bergmann

Viongozi hao Kansela Merkel, Rais Francois Hollande na Waziri Mkuu Matteo Renzi waliokutana kwenye kisiwa cha Ventotene,nchini Italia pia wamesisitiza kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kuwa imara.

Viongozi hao waliokutana kwenye manuwari katika mji huo wa Ventotene waliujadili mustakabal wa Umoja wa Ulaya baada ya Uingereza kuamua kujiondoa kwenye jumuiya hiyo. Wamesema jumuiya hiyo haitasambaratika baada ya Waingereza wa kupiga kura ya kuamua kujiondoa.

Mwenyeji wa mkutano Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi aliwaambia waandishi wa habari kwamba watu wengi walifikiri Umoja wa Ulaya utavunjika baada ya Waingereza kuamua kujitoa. Lakini amesema haijawa hivyo.

Waziri Mkuu Renzi ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya unauheshimu uamuzi wa Waingereza lakini sasa inapasa kuufungua ukurasa mpya wa mustakabal wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Italia Renzi amesema jambo la kipaumbele kwa Ulaya, sasa ni kuimarisha usalama wa ndani na wa nje kwa kushirikiana katika masuala ya upelelezi.

Hata hivyo Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametahadharisha juu ya hatari ya kutokea mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya mnamo siku za usoni. Hollande pia ameshauri mambo matatu muhimu,ikiwa pamoja na kushirikiana kwa undani zaidi, katika masuala ya usalama,kuhimiza vitega uchumi katika sekta za binafsi na umma na kuutekeleza mpango wa mafunzo ya kazi kwa vijana.

Kisiwa cha Ventotene ,ItaliaPicha: Max Hofmann

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza juu ya umuhimu wa kuustawisha uchumi ili kuleta neema na ajira kwa watu.

Katika mazungumzo yao viongozi wa Ujerumani,Ufaransa na Italia pia walizungumzia juu ya haja ya kuustawisha uchumi ili kuleta nafasi za ajira kwa watu Kansela Merkel na viongozi wenzake pia waliijadili migogoro ya dunia, kwenye mkutano wao wa Ventotene na hasa hatari ya ugaidi kutokana na mgogoro wa nchini Syria.

Merkel ametoa mwito wa kuchukua hatua zaidi za kuleta usalama wa ndani na wa nje ili kukubiliana na ugaidi.

Viongozi wa Ujerumani,Ufaransa na Italia, waliokutana kwenye kisiwa cha Ventotene pia waliweka mashada ya maua kwenye kaburi la msomi wa Kitaliani Altiero Spinelli anaezingatiwa kuwa mwasisi wa umoja wa Ulaya.

Mazumgumzo ya Kansela Merkel,Rais Hollande na Waziri Mkuu Matteo Renzi yalikuwa sehemu ya matayarisho ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika mjini Bratislava,nchini Slovakia mwenzi ujao.

Mwandishi:Mtullya Abdu.DW,afp,

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW