Mertesacker aamua kustaafu soka la kimataifa
16 Agosti 2014Beki huyo wa Arsenal ambaye aliisaidia Ujerumani kunyakua Kombe lake la nne la Dunia mwezi uliopita nchini Brazil, amefanya uamuzi huo kupitia mahojiano na televisheni ya ZDF na gazeti la kila siku la Süddeutsche Zeitung.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 amesema baada ya kuwa sehemu ya timu ya taifa kwa miaka kumi, ni kuhusu kuwa na uwezo wa kujiamulia wakati wa kuzitundika daluga.
Amesema ushindi wao wa Kombe la Dunia mwezi Julai ni “njia bora ya kustaafu” na sasa anataka kuzingatia tu mechi za ligi na kuisadia Arsenal kushinda mataji katika ligi kuu ya soka England na katika Champions League.
Kufuatia kujiuzulu kwa Miroslav Klose na nahodha Philipp Lahm, Mertesacker sasa ni mchezaji wa tatu kutundika njumu zake katikasoka la kimataifa kufuatia ushindi wa Die Mannaschaft nchini Brazil.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu