Merz aitetea bungeni bajeti ya serikali yake
24 Septemba 2025
Kansela Merz wa Ujerumani ametetea bajeti inayopendekezwa na serikali yake kwa kuliambia Bunge mjini Berlin kwamba hali ni ngumu kwa mataifa mengi ya Magharibi kutokana na misukosuko inayoshuhudiwa duniani.
Kimsingi Kansela Friedrich Merz amechagua kuchukua hatua yenye utata ya kubakia Berlin kushughulikia maswala ya ndani ya nchi yake badala ya kujiunga wiki hii na viongozi wengine wa dunia katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New -York, Marekani.
Na hasa ni kwa sababu ya suala muhimu la bajeti ya mwaka 2026 ambayo imependekezwa na serikali yake na inajadiliwa kwenye bunge la Ujerumani.
Katika hotuba yake mbele ya bunge amejikita zaidi kuelezea hali tete inayoshuhudiwa kimataifa akisema yamesababisha mtihani mkubwa kwa nchi zote za Magharibi:
"Kama taifa tunakabiliwa na mojawapo ya awamu za changamoto nyingi kabisa katika historia ya hivi karibuni. Hata hivyo sio nchi yetu tu inayoshuhudia hayo bali ni jamii nzima ya Magharibi ambayo maadili yake yanakabiliwa na majaribu ambayo pengine hayajawahi kushuhudiwa wakati mwingine. Na hili linaathari za moja kwa moja kwa uchumi unaojielekeza kwenye masoko ya dunia yanayotegemea sheria zinazotokana na miongozo ya ya kidunia ili kuweza kupata kikamilifu mafanikio ya ushindani''
Amewatanabahisha wabunge kwamba kukosekana kwa usalama kunatengeneza mazingira ya moja kwa moja ya kuathirika kwa uchumi wa Ujerumani ambayo tegemeo lake kubwa ni biashara ya nje:
"Sera za nje na za ndani haziwezi tena kutenganishwa. Narudia kuwaambia tena, ahadi zetu ikiwemo zangu binafasi katika sera za nje ziko kwa ajili ya kulinda uhuru amani na maendeleo pia na zaidi ndani ya nchi yetu mabibi na mabwana.''
Uchumi unaokuwa ndio utakaozalisha rasilimali zinazohitajika Ujerumani
Merz amesisitiza kwamba uchumi unaokuwa ndio utakaozalisha rasilimali zinazohitajika Ujerumani kusimamia miradi ya miundombinu, kuleta mshikamani na kuhakikisha usalama wa masuala ya ustawi wa kijamii kwa kipindi cha muda mrefu.
Pia ametahadharisha kwamba vyama vya wafanyakazi na waajiri wana wasiwasi kuhusu kupoteza ajira na kwahivyo amewahimiza wabunge kuchukua hatua za haraka kuliokoa taifa.
Lakini pia hakuacha kuvishambulia vyama vya upinzani vinavyoikosoa serikali yake kwamba inalenga kuondowa mfumo wa ustawi wa jamii.
Pamoja na kutowa mwito wa kupunguzwa gharama kwenye sekta ya usafiri wa anga, amekumbusha kwa kusisitiza kwamba bado sekta za magari, chuma na kemikali zitabakia kuwa muhimu kwa nchi hii ya viwanda.