Merz apata pigo uchaguzi wa jimbo la Baden-Württemberg
9 Machi 2026
Matokeo ya uchaguzi wa Jumapili yanaashiria pigo kwa kansela Merz kabla ya uchaguzi mwaka huu huku kura za maoni zikionyesha kuimarika kwa chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, AfD.
Karibu asilimia 32 ya wapiga kura walichagua chama cha Kijani kinachoongozwa na Cem Ozdemir, kulingana na kura za maoni baada ya vituo kufungwa zilizojumuishwa na vituo vya utangazaji vya ARD na ZDF, na kukishinda chama cha CDU kwa takriban asilimia 30.
Kura za maoni zilionyesha kuwa chama cha AfD kinakaribia mara mbili ya matokeo yake ikilinganishwa na uchaguzi wa 2021, kikishika nafasi ya tatu kwa takriban asilimia 18 ya kura.
Jimbo jirani na Baden-Wuerttemberg, Rhineland-Pfalz, litapiga kura katika wiki chache zijazo na Septemba kutakuwa na mfululizo wa kura za majimbo katika eneo la Ujerumani mashariki lililokuwa zamani chini ya utawala wa kikomunisti, ambako chama cha AfD kinaweza kutarajia kufanya vizuri.