Merz asema matendo ya Israel Gaza 'hayana tena uhalali'
26 Mei 2025
Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amesema Jumatatu kuwa "kiwango cha sasa cha mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza hakiwezi tena kuhalalishwa kama mapambano dhidi ya Hamas.”
"Kuumiza raia kwa kiwango kikubwa namna hii, kama ambavyo kumeongezeka siku za hivi karibuni, hakuwezi tena kuelezewa kama vita dhidi ya ugaidi wa Hamas,” alisema Merz katika mahojiano ya shirika la shirika la utangazaji la WDR.
Merz aliongeza kuwa anapanga kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wiki hii, kumtaka "asiende mbali kupita kiasi,” ingawa kwa sababu za kihistoria, Ujerumani huwa makini zaidi katika ukosoaji wake kuliko baadhi ya washirika wake wa Ulaya.
"Hata hivyo, kama mistari itavukwa, na sheria ya kimataifa ya kibinadamu ikakiukwa waziwazi, basi Ujerumani, na Kansela wa Ujerumani, lazima aseme jambo,” alisisitiza Merz.
Kauli zake zilitolewa kabla ya safari yake kuelekea Finland Jumatatu mchana, na zilikuja muda mfupi baada ya shambulio la Israel dhidi ya eneo linalowahifadhi wakimbizi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mapema asubuhi lililosababisha vifo vya watu kadhaa.
Jumatatu jeshi la Israel lilitoa amri kwa wakazi wa baadhi ya maeneo ya Khan Younis, kusini mwa Gaza kuhama, likidai kuwa makundi ya kigaidi yalirusha maroketi kutoka eneo hilo.
"Taasisi za kigaidi zinaendelea kurusha makombora kutoka maeneo yenu. Eneo la Khan Younis linachukuliwa kuwa uwanja wa mapigano hatarishi na tayari limeonywa mara kadhaa,” ilisomeka taarifa kwa lugha ya Kiarabu. "Hamieni mara moja kuelekea magharibi, katika eneo la Mawasi,” taarifa hiyo iliongeza.
Mkuu wa shirika jipya la misaada Gaza ajiuzulu kwa sababu za kimaadili
Shirika la 'Gaza Humanitarian Foundation' linatarajiwa kuanza kazi Jumatatu, licha ya kujiuzulu kwa Mmarekani aliyekuwa akiongoza juhudi hizo.
Jake Wood alijiuzulu Jumapili, akieleza kuwa mpango mpya wa msaada hautamruhusu kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.
"Ni wazi kuwa haiwezekani kutekeleza mpango huu huku nikizingatia kikamilifu misingi ya kibinadamu ya utu, kutokuegemea upande wowote, usawa, na uhuru wa kujitegemea — misingi ambayo siwezi kuiacha,” alisema katika taarifa.
Israel imeishtumu Hamas kwa kuingilia misaada hiyo, lakini Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya misaada wamekanusha kuwepo kwa udanganyifu mkubwa.
Umoja wa Mataifa pia umekataa mpango wa Israel wa kusambaza msaada kupitia wakfu huo mpya wa Gaza Humanitarian Foundation.
UN imesema mpango huo unairuhusu Israel kutumia chakula kama silaha, kwani utawalazimisha raia kutembea umbali mrefu kupitia maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Israel ili kupata msaada wa chakula.
Israel ilikuwa imezuia kuingia kwa chakula, mafuta, dawa na vifaa vingine vyote kwa karibu miezi mitatu, kabla ya kuruhusu kiasi kidogo cha misaada wiki iliyopita, baada ya jumuiya ya kimataifa kupiga kelele na kuonya juu ya baa kali la njaa.
Gaza Humanitarian Foundation ilianzishwa mwezi Februari, na inaungwa mkono na serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump.