Merz asema Ujerumani haitojiunga sasa na Bodi ya Amani
24 Januari 2026
Kiongozi huyo hata hivyo ameonyesha utayari wa kushiriki katika mifumo mipya ya mazungumzo na Marekani.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana mjini Roma nchini Italia baada ya mazungumzo kati ya maafisa wa serikali za Ujerumani na Italia, Merz alisema wako tayari kutafuta aina nyingine mpya za ushirikiano na Marekani.
Merz alisisitiza kwamba wiki zilizopita, alimueleza Trump nia yake binafsi ya kushiriki katika chombo kama hicho lakini akaongeza kuwa kwa muundo wake wa sasa, hakiwezi kukubaliwa na Ujerumani kwa sababu za kikatiba.
Hata hivyo, Merz amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Marekani linapokuja suala la "kutafuta muundo mpya" ambao unaleta amani karibu katika maeneo mbalimbali ya dunia na sio tu kwa Gaza na Mashariki ya Kati lakini inaweza pia kwa Ukraine.