Merz: Dunia imeingia katika "enzi ya siasa za nguvu kubwa"
22 Januari 2026
Merz amesema utaratibu wa kimataifa uliodumu kwa miongo kadhaa sasa "unaporomoka kwa kasi ya kutisha," na kwamba mataifa ya Ulaya hayana budi kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na mazingira mapya ya kisiasa na kiusalama.
"Tumeingia katika enzi ya siasa za nguvu kubwa. Utaratibu wa kimataifa wa miongo mitatu iliyopita, uliotegemea sheria za kimataifa, haujawahi kuwa mkamilifu. Leo, misingi yake yenyewe imetikisika."
Kansela huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa dunia imeingia katika "enzi ya siasa za nguvu kubwa," akitaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kama tukio lililoashiria mwanzo wa sura mpya katika siasa za kimataifa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mabadiliko yanayoendelea ni mapana zaidi ya mgogoro wa Ukraine, yakihusisha mabadiliko ya mizani ya nguvu duniani na kuongezeka kwa ushindani kati ya mataifa makubwa.
Merz ameyasema hayo saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kubadili msimamo wake kuhusu Greenland, akiondoa vitisho vya kutumia nguvu kuipata na kuahidi kutoweka ushuru mpya kwa baadhi ya nchi za jumuiya ya kujihami ya NATO ikiwemo Ujerumani.