1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Merz kujadili vita vya Ukraine wakati wa ziara yake China

20 Februari 2026

Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Sebastian Hille amesema vita vya Urusi na Ukraine vitakuwa katika ajenda ya mazungumzo wakati atakaposafiri kuelekea China katika ziara yake ya kwanza rasmi nchini humo.

Picha ya pamoja I China Xi,Ujerumani Merz
Picha ya Pamoja ya Rais wa China Xi Jinping na Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Li Xueren/Xinhua/-,Yauhen Yerchak/Zuma Wire/picture-alliance

Sebastian Hille hakutoa maelezo zaidi juu ya ziara hiyo. 

Katika ziara yake ya kwanza rasmi nchini China, Merz anatarajiwa kuwa makini katika maongezi yake ambako kwanza atalazimika  kuihakikishia China kwamba ni mshirika muhimu kwa Ujerumani na pili atakuwa pia na jukumu la kuyaangazia pia masuala mbali mbali ikiwemo usalama, siasa za kimaeneo, biashara na haki za binadamu.

Hille amethibitisha hilo kwa kusema kuwa masuala ya mahusiano ya pande mbili China na Ujerumani, uchumi na usalama ni mambo yatakayokuwa katika ajenda ya mazungumzo. Ameongeza kuwa Kansela Merz atasafiri China na wajumbe kadhaa wa biashara. 

Katika safari yake hiyo itakayofanyika siku ya Jumatano wiki Ijayo, anatarajiwa kupokewa mjini Beijing na Waziri Mkuu Li Qiang kabla ya kukutana na Rais Xi Jinping baadae kabla ya kula pamoja chakula cha jioni.

EU yapanga kuiwekea vikwazo zaidi Urusi 

Haya yanajiri wakati mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, akitangaza kuwa Umoja huo unapanga kupitisha duru ya 20 ya vikwazo dhidi ya Urusi siku ya Jumatatu (23.02.2026), wiki ijayo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja KallasPicha: Wojtek Radwanski/AFP/Getty Images

Taarifa yake inakuja licha ya wajumbe wa EU kushindwa siku Ijumaa kuidhinisha vikwazo hivyo ambavyo vingejumuisha marufuku kamili ya huduma za baharini kwa usafirishaji wa mafuta ghafi ya Urusi.

Kallas amesema vikwazo vinafanya kazi na kwa sasa vinaudhoofisha uchumi wa Urusi na kila hatua zaidi zinazochukuliwa zinadhibiti na kupunguza nguvu zake katika vita vyake Ukraine. 

Aidha mawaziri wa mambo ya nje wa EU wanatarajiwa kukutana siku ya Jumatatu mjini Brussels kujadili vikwazo hivyo pamoja na masuala mengine muhimu.

 

 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW