1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz yuko China kujadili, Ulinzi, uchumi na vita vya Ukraine

Amina Abubakar dpa/reuters
25 Februari 2026

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz yuko nchini China kwa ziara yake ya kwanza ya siku mbili tangu alipochaguliwa kuwa Kansela katikati ya mwaka Jana. Merz atajadili mambo mengi ikiwemo Ukraine, uchumi na ulinzi.

China 2026 | Friedrich Merz na Li Qiang
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akiwa na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wakati akimpokea mjini Beijing. Merz yuko China kwa ziara ya siku mbili. Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Merz ameanza ziara yake katika nchi hiyo iliyo mshirika wake mkubwa wa kibiashara na mshindani wake mkuu katika masuala ya teknolojia. Ziara hiyo pia inafanyika wakati uchumi wa Ujerumani ulio mkubwa zaidi barani Ulaya ukitikisika.

Ujerumani na China zinataka kuimarisha mahusiano yao ya kiuchumi wakati ambapo rais wa Marekani Donald Trump akiwa amesababisha mvutano mkubwa wa kibiashara duniani kutokana na hatua zake za ongezeko la ushuru na mabadiliko ya sera zake za kigeni.

Katika Mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa China Li Qiang, Merz alisema kwamba Ujerumani inataka kuimarisha mahusiano yake ya kiuchumi huku ikisisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa haki na wa wazi.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

"Tunataka ushirikiano na China. Ushirikiano ulio na usawa, wa kuaminika na wa haki. Hayo ndio tunayoyataka na kuyaomba. Na pia tunatumai na kutarajia hayo hayo kutoka upande wa China."

Li hata hivyo ametoa wito kwa pande zote mbili kufanya kazi pamoja kulinda ushirikiano na biashara huria na kujitahidi pia kujenga mfumo wa uongozi wa biashara uliyo na haki duniani.

Uchumi wa Ujerumani unaoongozwa na mauzo ya nje, umekuwa ukitegemea zaidi soko kubwa la China katika miaka ya hivi karibuni, lakini pia mauzo ya bidhaa za Ujerumani kama vile magari yamepungua kutokana na ushindani wa ndani unaoongezeka.

Merz kuzungumza na Xi kuhusu Ukraine

Hii leo jioni Kansela huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuzungumza na rais wa China ,Xi Jinping katika majadiliano yatakayogusia masuala ya ulinzi, na pia haki za binaadamu. Merz pia anatarajiwa kusisitiza masilahi ya Ujerumani na Ulaya kwa kumuomba amshinikize mshirika wake mkubwa Urusi kusitisha vita vyake Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz akiwa na rais wa China Xi Jinping wakiwa mjini Beijing Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

China ambaye ni taifa la pili kubwa kiuchumi duniani, liliipiku Marekani mwaka uliyopita kwa kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Ujerumani, lakini licha ya hilo ujerumani inaliona taifa hilo linalotawaliwa na chama cha kikomunisti kuwa mpinzani wa kimfumo wa Ulaya.

Merz yuko katika  ziara yake hiyo ya siku mbili akiwa ameandamana na Ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara 30 wa Ujerumani Ujerumani wakiwemo wakuu wa kampuni za magari za Volkswagen, BMW na Mercedes-Benz.

Kampuni hizi ni sehemu ya zile ambazo zimejikuta zikibanwa katikati kwenye ushindani wa kibiashara baina ya ukuwaji mkubwa wa sekta ya viwanda vya magari ya umeme ya China na vikwazo vya ushuru vya Marekani, ambavyo vimeongeza gharama za mabilioni upande wao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW