Mesut Özil awashukuru mashabiki wa Real
4 Septemba 2013"Asanteni sana kwa miaka mitatu murwaa kabisa na nyinyi nyote. Wakati wangu ulikuwa wa kipekee na maalumu sana kwangu. Wakati mwingine mambo yanakwenda tofauti na vile nilivyotarajia siku chache zilIzopita," amesema Özil katika taarifa yake aliyoitoa Jumatatu usiku (02.09.2013) baada ya uhamisho huo.
"Nawatakieni nyote pamoja na timu kila la kheri. Sasa nina matarajio makubwa na klabu yangu mpya: Wabeba Bunduki - Arsenal!" Mchezaji huyo wa miaka 24 pia aliweka bayana siku ya Jumanne kwenye mahojiano na televisheni ya shirikisho la soka la Ujerumani, dfb-tv, kuwa wakati unafaa kuondoka Madrid kwa kuwa haonekani akifaa katika mipango ya kocha mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti. "Niligundua katika siku za hivi karibuni sikuwa na uaminifu wa kocha. Arsenal wana imani hiyo na mimi kwa hiyo nitakwenda kujiendeleza zaidi," amesema Özil.
Özil ni mchezaji wa Ujerumani anayelipwa kitita kikubwa
Arsenal ililipa rekodi ya paundi milioni 42.5, sawa na dola milioni 66, kwa kiungo huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano. Özil anajiunga na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Ujerumani, Per Mertesacker na Lukas Podolski katika klabu ya Arsenal na atavaa jezi nambari 11 mgongoni. Kiwango hicho ni kikubwa kuwahi kulipwa kwa ajili ya mchezaji wa soka wa Ujerumani, kupita kile cha euro milioni 37 ambacho mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani, Bayern Munich, waliilipa Borussia Dortmund kumpata Mario Goetze mapema mwaka huu.
Özil pia amekuwa mchezaji aliyeuzwa kwa gharama kubwa na Real Madrid. Rekodi iliyokuwepo ilikuwa ikishikiliwa na mshambuliaji kutoka Brazil, Robinho, ambaye alihamia Manchester City mwaka 2008 kwa kitita cha euro milioni 43. Kuondoka kwa Özil kulikamilishwa baada ya kuthibitishwa uhamisho wa Gareth Bale hadi Real Madrid kutoka kwa mahasimu wa Arsenal wa kaskazini mwa jiji la London, Tottenham Hotspur. Uhamisho huo uliweka rekodi mpya ya euro milioni 100.
Hatua ya Özil kuhamia Arsenal haingeweza kuepukika baada ya Real Madrid kukataa kutilia maanani ombi la mchezaji huyo kutaka aongezwe mshahara. Mashabiki wengi wa Real Madrid wametamaushwa na uhamisho wa Özil huku asilimia 66 walioulizwa kwenye utafiti wa maoni katika mtandao wa intaneti uliofanywa na gazeti la michezo la As wakipinga uhamisho huo.
Mwandishi: Josephat Charo/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga