Meya wa Berlin asema Novemba 9 ni muhimu kwa hali zote
9 Novemba 2024Katika hafla ya kuadhimisha miaka 35 tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, iliyohudhuriwa na Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani, meya huyo alisema siku hii inaadhimisha matukio mawili makubwa, ambayo ni kuanguka kwa ukuta huo mwaka 1989 na mwazo wa wimbi la hofu lililoongozwa na Wanazi dhidi ya Wayahudi mwaka 1938 ambalo baadaye lilijulikana kama usiku wa Kristallnacht.
Soma zaidi: Mamilioni ya Wajerumani Mashariki wahamia Magharibi
Akizungumzia kuanguka kwa ukuta wa Berlin, Wegner amesema nyakati hizo zilikuwa na kusisimua wakati watu walipousukuma ukuta na kuhitimisha enzi ya utengano na kufungua njia ya kuungana tena kwa iliyokuwa Ujerumani Magharibi na Mashariki.
Amesema anatumai kwamba matumaini na mshikamano uliokuwepo wakati huo utarejea Ujerumani huku akisisitiza uhumuhimu wa uhuru, akiwatolea mwito wajerumani kuudumisha akisema bila uhuru kila kitu kinakosa maana.
"Berlin haijagawanyika kwa miaka 35. nchi yetu imeungana, Ulaya imeungana. Lakini bado kuna watu wengi na nataka kuwakaribisha wote hapa hii leo, wale wasioishi kwa uhuru na demokrasia, wale ambao bado wanapigana. na naweza kuwambia kuwa Berlin inajivunia kuwa mji huru. Na nataka Berlin kuwa eneo la matumaini, eneo la matumaini kwa watu wote ambao bado hawaishi huru lakini ambao wanapigania uhuru wao." Alisema meya huyo.
Baadaye jioni kulitarajiwa kuwapo na onesho la burudani ya muziki na uwashaji wa taa kwenye lango mashuhuri la Brandeburg mjini Berlin, eneo ambako Ukuta wa Berlin ulikatisha na kuzitenganisha pande mbili za mji huo mkuu tangu mwaka 1961.