1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meya wa jiji la Dar es Salaam avuliwa madaraka

Sylvia Mwehozi
9 Januari 2020

Katika kile kinachoonekana kama muendelezo wa kuwaondoa viongozi wa kuchaguliwa kutoka upinzani kwenye nafasi zao nchini Tanzania, meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amevuliwa madaraka.

Isaya Mwita ehemaliger Bürgermeister in Daressalam
Picha: S. Khamis

Meya huyo, Isaya Mwita, anayetoka chama kikuu cha upinzani cha Chadema, amevuliwa wadhifa huo katika kikao kilichotawaliwa na vurugu, baada ya madiwani wa upinzani kudai kulikuwa na udanganyifu kwenye orodha ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Karemjee.

Mara baada ya hatua hiyo ya kumuondoa kufanyika, Meya Mwita alizungumza na waandishi wa habari kwa hisia kali, huku akiwataka viongozi wa dini kumwombea kutokana na yale anayopitia, na akiapa kupigania haki yake ya kuwa meya halali wa Dar es Salaam hadi dakika ya mwisho: "Bado mimi ni meya kwasababu kikao ambacho kimefanyika hapa kimepata dosari mbili ya kwanza tumepata changamoto ya udanganyifu wa jina la Mshamu aliye nje ya nchi, na mimi mara baada ya kufika hapa nilimueleza makamu kama mko na akidi mnaweza kuendelea, kumbe hawakuwa na akidi", alisema meya huyo.

Kulingana na hoja zake, kukosekana kwa akidi ya wajumbe waliopaswa kupiga kura ili aondolewe madarakani ndiyo sababu inayompa nguvu ya kupinga maamuzi ya kikao hicho na kufanya aendelee kujitambua bado ni meya. Ameapa kwenda mahakamani kutetea nafasi yake hiyo:

Rais wa Tanzania John Magufuli Picha: DW/E. Boniphace

Imefahamika kuwa mara tu baada ya uamuzi huo kuchukuliwa na kikao cha madiwani 16 wa chama tawala cha Mapinduzi, CCM, Meya Mwita alinyang'anywa gari alilokuwa akitumia na pia ofisi yake ya umeya kufungwa. Baadhi ya hoja zilizotumiwa na madiwani wa CCM kumuondoa meya huyo wa upinzani ni pamoja na ile inayosema dereva wake alipata ajali kwa kutumia gari hiyo na pia mwenyewe alihusika na ubadhirifu wa takribani shilingi bilioni tano za umma - mambo ambayo anayakana.

Ufafanuzi wa kisheria

DW imezungumza na mwanasheria Jebra Kambole kutaka ufafanuzi wa kisheria juu ya hatua hiyo na amesema kuwa "jambo hili tayari lilikuwa mahakamani, lilitakiwa liongozwe na tume na baraza lililokuwa linataka kumuondoa, lakini pia lazima meya asikilizwe vizuri kabla ya kuondolewa. Lazima akidi itimie kabla mtu hajachukuliwa sheria na lazima jambo hili liheshimiwe," amesema mwanasheria huyo aliyeko nchini Tanzania. 

Kuondolewa kwa meya huyo sasa kunafanya miji iliyokuwa ikidhibitiwa na wapinzani kurejea mikononi mwa chama tawala CCM, na hii imechangiwa na hatua ya baadhi ya wabunge na madiwani kuvihama vyama vyao na kujiunga na chama hicho tawala.

Hivi karibuni pia meya wa jiji mashuhuri kwa utalii na biashara kaskazini mwa Tanzania, Arusha, naye alifuata mkondo wa wanasiasa waliotangulia wa kuvihama vyama vyao na kwenda CCM.  Katika uchaguzi uliopita wa 2015, wapinzani walifanikiwa kudhibiti maeneo mengi yakiwamo kushinda ubunge na udiwani katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam na Arusha.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW