1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu Liz Truss na safari yake kisiasa

6 Septemba 2022

Liz Truss anatumai kuwa kama waziri mkuu wa zamani Margaret Thatcher aliyeurudisha uchumi wa Uingereza katika hali nzuri ya ukuaji mnamo miaka ya 1980 kufuatia hatua zake za ubinafsishaji na kupunguza udhibiti.

Liz Truss Premierministerin UK
Picha: Frank Augstein/AP/picture alliance

Hakika yeye si mgeni wa vitimbi au vichekesho vya kisiasa: Katika mkutano wa chama cha Kihafidhina mwaka 2014, alipozungumza kama Waziri wa Mazingira, Chakula na Masuala ya Vijijini, Liz Truss ambaye sasa ana umri wa miaka 47, alizungumzia ubora wa vyakula vya Uingereza, ngano ya Uingereza na uuzaji wa chai ya Yorkshire kwa China. Lakini ghafla akadai kuwa Uingereza inaagiza theluthi mbili ya jibini kutoka nje: "Hiyo ni aibu!” Nusura wajumbe wa chama wasakamwe na mkate wa sandwichi.

Kuna wakati pia aliulizwa bungeni kuhusu hatua zinazochukuliwa kukabili droni zinazotumiwa kuingiza dawa magerezani kimagendo. Truss alijibu kuwa wapo mbwa maalum magerezani na mibweko yao husaidia kuzuia droni hizo.

Mitandaoni kuna video chungu nzima ya kauli zake za kuchekesha ambazo wakosoaji wake wanatumia kutilia shaka uwezo wake wa kiakili na iwapo anafaa kuwa waziri mkuu.

Amethibitisha kuwa msanii aliyeponea kutimuliwa katika serikali za kihafidhina katika miaka 12 iliyopita. Ameendelea kukua kisiasa akishika nyadhifa mbalimbali katika wizara ya Sheria, Fedha, Biashara ya kimataifa hadi wizara ya Mambo ya Nje.

Anayebadili misimamo ya kisiasa?

Truss ajitizama kama mrithi wa Margaret Thatcher aliyeisaidia nchi hiyo kujinasua kutoka kwenye hali ngumu za kiuchumi katika miaka ya 80.Picha: Peter Nicholls/REUTERS

Japo wengi wa waliokuwa mawaziri wenzake wametimuliwa kufuatia cheche na mivutano ya ndani ya chama, yeye alinusurika. Wengi walipojiuzulu kufuatia kuondoka kwa Waziri Mkuu wa zamani Theresa May, yeye alisalia, na hata Boris Johnson alipofanya mabadiliko makubwa ya mwisho kwenye serikali yake, Truss hakuathiriwa. Ameonekana kuwa mtiifu na afanyaye kazi kwa bidii, lakini hii ni bila ya yeyote kumuweka kwenye mizani kubaini kama kweli amefanikisha lolote.

Awali aliunga mkono Uingereza kusalia katika Umoja wa Ulaya, lakini baada ya kura ya Brexit, amegeuka kuwa mtetezi mkubwa wa Brexit. Aidha katika miaka michache iliyopita Truss amekuwa akiegemea zaidi siasa za mrengo wa kulia, kiasi kwamba anatizamwa kuwa mkereketwa zaidi wa misimamo halisi ya wahafidhina, jambo linaloungwa mkono na wanachama hasa katika ngome zao za tangu zamani kusini mwa England.

Ataka kufuata nyayo za Margaret Thatcher

Anatumai kuwa kama mrithi wa waziri mkuu wa zamani Margaret Thatcher aliyeurudisha uchumi wa Uingereza katika hali nzuri ya ukuaji mnamo miaka ya 1980 kufuatia hatua zake za ubinafsishaji mkubwa na kupunguza udhibiti.

Truss anataka kupunguza viwango vya sasa vya mfumuko wa bei za bidhaa kwa kupunguza kodi, hata kama maafisa wa uchumi katika Benki Kuu ya England wanapinga, kwa kuhofia itaongeza bei ambayo tayari imeshapanda.

Truss anasisitiza kwamba shuruti kuwe na usambazaji zaidi kwenye soko la nishati. Ananuwia kuwa na makubaliano kadhaa kuhusu mafuta na gesi katika Bahari ya Kaskazini.Picha: Clodagh Kilcoyne/REUTERS

Mtafiti wa masuala ya uchumi Simon Lee wa Chuo Kikuu cha Hull, pia anaamini ni jambo la kawaida kutarajia serikali ya Uingereza kuwapa mamilioni ya watu binafsi, familia na kampuni, msaada wa moja kwa moja wanaohitaji wa kifedha ili kustahimili gharama ya maisha. Anasema katika mgogoro wa kifedha ulioikumba Uingereza mwaka 2008, nchi hiyo ilitumia pauni trilioni mbili kuzuia uchumi wa nchi kuporomoka.

Je mpango wake kwa kaya zinazolemewa na gharama za maisha ni upi?

Hata hivyo ameliacha wazi swali la ni vipi anapanga kuzisaidia familia maskini, akisema huo utakuwa wajibu wa waziri mpya wa fedha. Lakini ataweza tu kuongeza mabilioni ya fedha yanayohitajika kwa kuchukua mikopo zaidi. Deni la taifa la Uingereza lilipanda kwa kasi wakati wa janga la virusi vya corona. Ikiwa mipango mingine mikubwa ya misaada itahitajika basi mzigo utaongezeka kwa serikali.

Anatarajiwa kuwasilisha bajeti yake kadri anavyoanza majukumu yake rasmi. Lakini amewahi kusema kodi za chini zitahakikisha wengi wana pesa mifukoni mwao.

Truss anasisitiza kwamba shuruti kuwe na usambazaji zaidi kwenye soko la nishati. Ananuwia kuwa na makubaliano kadhaa kuhusu mafuta na gesi katika Bahari ya Kaskazini.

Kuhusu sera ya kigeni, ni bayana kuwa Truss anakusudia kutafuta ugomvi na Umoja wa Ulaya kufuatia nia yake ya kufutwa mara moja kwa itifaki ya Ireland Kaskazini kutoka makubaliano ya Brexit.

https://p.dw.com/p/4GMYH

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Grace Patricia Kabogo