1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Charles III afungua mkutano wa kilele wa Commonwealth

25 Oktoba 2024

Mfalme Charles wa Tatu wa Uingereza ameufungua mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola nchini Samoa hivi leo, akikiri dhuluma za kihistoria zilizofanywa na Himaya ya Uingereza kwenye masuala ya utumwa.

Mfalme Charles III wa Uingereza na mkuu wa Jumuiya ya Madola.
Mfalme Charles III wa Uingereza na mkuu wa Jumuiya ya Madola.Picha: Lukas Coch/AP Photo/picture alliance

Mfalme huyo, ambaye anawakilisha taifa lililotenda unyama na ukatili mkubwa dhidi ya mamilioni ya watu duniani, amewaambia viongozi wa mataifa yanayounda Jumuiya ya Madola kwamba yaliyopita hayawezi kubadilishwa.

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo wa Jumuiya ya Madola mjini Apina, Mfalme Charles alionekana kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutambua miito kutoka baadhi ya makoloni ya zamani ya Uingereza kumtaka mkoloni huyo abebe jukumu kwa dhima yake kwenye biashara katili ya utumwa wa Bahari ya Atlantiki.

"Mshikamano wetu unahitaji tutambuwe tulikotoka. Ninafahamu kutokana na kuwasikiliza watu kote kwenye Jumuiya ya Madola, kwa jinsi gani matukio yenye maumivu makali sana kwenye historia yetu yanavyoendelea kutuandama." Alisema Mfalme Charles.

Soma zaidi: Viongozi wa Afrika waomboleza kifo cha Malkia Elizabeth II

"Kwa hivyo, ni muhimu kwamba tunaielewa historia yetu ili ituongoze kwenye maamuzi sahihi huko twendako. Hakuna anayeweza kubadilisha yaliyopita miongoni mwetu, lakini tunaweza kujitolea kwa moyo wote kujifunza na kusaka njia za kurekebisha ukosefu wa usawa tunaokabiliana nao." Aliongeza.

Mfalme Charles III wa Uingereza na mkuu wa Jumuiya ya Madola.Picha: Chris Jackson/PA/empics/picture alliance

Kauli ya Mfalme Charles, ambaye anahudhuria kwa mara ya kwanza mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola akiwa mfalme, ilikinzana na Waziri Mkuu wake, Keir Starmer, ambaye hapo jana alisema mkutano huu ulitakiwa uepuke kutandwa na mijadala mirefu isiyokwisha kuhusu fidia ya utumwa.

Starmer alisema ajenda ya utumwa isingelikuwamo kabisa kwenye mkutano huu, ingawa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland, aliliambia shirika la habari la AP kwamba viongozi watasema chochote wanachotaka kwenye mkutano wa siku nzima wa faragha kesho Jumamosi.

Mataifa ya Karibiani yaja juu

Mataifa ya Karibiani kwenye Jumuiya hiyo iliyoundwa makhsusi kudumisha mafungamano ya Uingereza na makoloni yake yamekuwa yakisema wazi kwamba suala la utumwa lazima lizungumzwe na limalizwe, wakimaanisha kuwe na tamko la kuombwa radhi na pia fidia kwa wahanga wa ukatili huo dhidi ya ubinaadamu. 

Mfalme Charles III wa Uingereza na mkuu wa Jumuiya ya Madola na mkewe Camilla.Picha: Chris Jackson/PA/empics/picture alliance

Waziri Mkuu wa Bahamas, Phillip Davis, alisema hapo jana kwamba anataka mjadala wa wazi na Starmer juu ya suala hili na atahakikisha kuwa kwenye tamko la mwisho la mkutano huo wa kilele wa Jumuiya ya Madola, munawekwa kipengele maalum cha fidia. 

Soma zaidi: Mkutano wa 55 wa Jumuiya ya Madola mjini Arusha,Tanzania

Uingereza haijawahi kuomba radhi rasmi kwa dhima yake kwenye biashara hiyo, ambayo ilishuhudia mamilioni ya raia wa Afrika wakitekwa na kupelekwa kwenye mashamba makubwa ya kilimo katika maeneo ya Karibiani na Amerika kwa karne kadhaa, na kuzitajirisha familia na kampuni za Uingereza, zikiwemo familia za kifalme na mabwanyenye wa sasa.

Utafiti uliofanywa na wafuatiliaji wa masuala ya fidia za kihistoria unasema Uingereza inadaiwa baina ya mamilioni na matrilioni ya dola na vizazi vya watumwa hao.