1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mfalme Charles III agunduliwa na saratani

6 Februari 2024

Utawala wa Kifalme nchini Uingereza umetangaza kuwa Mfalme Charles III amegunduliwa kuwa na saratani lakini bila kufafanua aina ya saratani iliyopatikana.

Uingereza
Mfalme Charles III wakati wa mazishi ya mama yake Malkia Elizabeth II.Picha: Alkis Konstantinidis/Pool photo via AP/picture alliance

Mamlaka ya Kasri la Buckingham imeeleza kuwa saratani hiyo iligundulika wakati wa matibabu ya kawaida ya tezi dume na kwamba kwa sasa Mfalme huyo ameanza kupatiwa matibabu na atahitaji kupumzika.

Mfalme Charles wa tatu amekula kiapo na amevikwa taji kwenye sherehe iliyohudhuriwa na maalfu ya wageni na watu mashuhuri.

Charles mwenye umri wa miaka 75, ambaye alikua mfalme baada ya kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II, mnamo Septemba 8, 2022, aliyeiaga dunia akiwa na umri wa miaka 96.

Taarifa kutoka Kasri la Buckingham imesema mfalme Charles III "anaendelea kuwa na matarajio chanya" kwamba atarejea kikamilifu katika shughuli za umma haraka iwezekanavyo. Hii ni baada ya Mfalme huyo kushauriwa na madaktari asitishe kushughulikia kazi za umma, ingawa anaweza kuendelea kufanya shughuli za serikali kama kawaida.

Soma pia: Mfalme Charles III ziarani Kenya

Shifaa ya haraka

Mfalme Charles akitoka katika hospitali ya London ambapo amekuwa akipokea matibabu ya uvimbe wa tezi dume.Picha: Victoria Jones/empics/picture alliance

Tangazo hilo la kuungua kwa Mfalme Charles III liliibua mwamko wa mshikamano na uungwaji mkono, Mwanamfalme Harry akisema amezungumza na baba yake na atamtembelea hivi karibuni. Mrithi wa kiti cha enzi Mwanamfalme William, anatarajiwa kutimiza baadhi ya majukumu ya mfalme wakati anapoendelea na matibabu.

Aidha taarifa ya Ikulu imepongeza kusema kwamba mfalme alichagua kuweka wazi matokeo ya uchunguzi wake wa saratani "ili kuzuia uvumi na matumaini kwamba inaweza kusaidia uelewa wa umma kwa wale wote ulimwenguni ambao wameathiriwa na saratani".

Mwezi uliopita Mfalme Charles alipongezwa kwa kuwa muwazi juu ya hali ya matibabu ya uvimbe wa tezi dume, na madaktari wakisema kuwa watu wengi zaidi wenye dalili hizo wamekuwa wakijitokeza.

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema "ameshtushwa na kuhuzunishwa" na habari hizo, lakini amefarijika kwamba ugonjwa huo umegundulika mapema.

Kupitia mtandao wa X Sunak ameandika nikumnukuu "Namtakia Mfalme apate nafuu kamili na ya haraka. Sina shaka kuwa atarejea kwa nguvu zote muda si mrefu na najua nchi nzima itamtakia heri." mwisho wa nukuu.

Viongozi mbalimbali duniani wakiwemo rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na wengine kadhaa, wametuma pia salamu za kumtakia ahueni Mfalme Charles III.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW