1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mfalme Charles III amkaribisha rasmi Trump

17 Septemba 2025

Sherehe na shamrashamra za mapokezi ya kifalme kwa Rais Donald Trump wa Marekani zimefanyika katika Kasri la Windsor nchini Uingereza hivi leo, zikipambwa kwa gwaride maalum, magari ya farasi na zumari.

Uingereza Windsor 2025 | Ziara ya Donald Trump kwa Mfalme Charles III
Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) akiwa na mwenyeji wake, Mfalme Charles III (katikati), wakikaguwa gwaride rasmi katika Kasri la Windsor, London, Uingereza.Picha: Kirsty Wigglesworth/AFP

Haya yanatajwa kuwa mapokezi ya kifakhari na anasa zaidi kuwahi kufanyika kwa kiongozi wa taifa la nje nchini Uingereza katika miaka ya hivi karibuni.

Jumla ya farasi 120 na wanajeshi 1300 wa Uingereza - wengine wakivalia mavazi ya asili ya sare nyekundu na makofia makubwa yenye urinda wa dhahabu - walionesha ujuzi wao mbele ya Trump kwenye gwaride kubwa la heshima. 

Mrithi wa kiti cha ufalme William na mkewe Catherine waliwapokea kwa uchangamfu Trump na mkewe, Melina, mara tu baada ya helikopta ya jeshi la anga kutuwa kwenye viwanja cha Windsor majira ya saa 6:15 mchana wa Jumatano (Septemba 17).

Ndani ya uwanja uliozungukwa na makuta manene ya kasri hilo na mbali kabisa na waandamanaji, William na Catherine waliwasindikiza Trump na Melina na kwenda kumuamkia Mfalme Charles na mkewe Camilla. 

Trump, Charles wachangamkiana

Wakati Trump alipopeana mkono na Charles, mizinga 41 ya heshima ilipigwa kwa pamoja kutoka bunduki sita zilizotumika katika Vita vya Kwanza vya Dunia katika eneo la magharibi mwa kasri hilo, kama vile ilivyoonekana kwenye Mnara wa London katikati mwa mji mkuu huo wa Uingereza.

Mrithi wa Ufalme wa Uingereza, William (kushoto), akimkaribisha Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Aaron Chown/PA Wire/dpa/picture alliance

Kisha akina Trump na Charles walipanda kwa pamoja gari la farasi kuzunguka kasri na baadaye kukaguwa gwaride la heshima. 

Wawili hao walionekana kila mara wakitaniana na kucheka kwa pamoja, na Rais Trump akipiga saluti  wakati wimbo wa taifa wa Marekani ulipopigwa kabla yeye na wenyeji wake kuelekea kwenye tafrija ya chakula cha mchana.

Wadadisi wa mambo wanasema Uingereza imechupa mpaka kwenye juhudi zake za kumpendeza na kumridhisha Trump asiyetabirika wakati huu kiongozi huyo akiwa kwenye kiini cha mizozo mikubwa duniani.

Mbali na macho ya raia wa kawaida

Kwa kiasi kikubwa, serikali ya Uingereza imefanikiwa kumuweka Trump mbali na macho ya raia wa kawaida, lakini nje ya Kasri la Windsor, waandamanaji walikuwa wanapaza sauti zao kupinga ziara hii, wakisema Trump si mgeni "mwenye heshima ya kukaribishwa" nchini mwao.

Miongoni mwa waandamanaji waliokusanyika nje ya Kasri la Windsor kumpinga Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Jack Taylor/Getty Images

"Tunafanya maandamano haya leo kwa kuwa tunataka kuwapa nafasi watu wengi wa Uingereza kuelezea hisia zao juu ya ukweli kwamba wanamchukia Donald Trump. Wanachukia siasa zake, wanachukia ubagazi wake wa rangi, ukweli kwamba yeye ni mbakaji, ukweli kwamba anayawezesha mauaji ya kimbari huko Gaza, ukweli kwamba anasuhubiana na Putin. Zote hizi ni siasa zinazowachafua watu wa Uingereza." Alisema Zoe Garnder anayeongoza kundi liitwalo Stop Trump Coalition.

Trump ni rais wa kwanza wa Marekani kupata bahati ya kuitembeleaUingereza mara mbili kwa mualiko wa kifalme, mara ya kwanza ikiwa mwaka 2019 alipoalikwa na Malkia Elizabeth wa Pili, mama yake Mfalme Charles.

Atakuwa pia rais wa kwanza kushuhudia gwaride la pamoja la ndege za kijeshi za Marekani na Uingereza, na kisha kuweka shada la mauwa kwenye kaburi la Malkia Elizabeth aliyefariki dunia mwaka 2022.