Mfalme Charles lll kuendeleza amani ya Ireland Kaskazni
13 Septemba 2022Mfalme Charles wa tatu baada ya kuwasili Ireland Kaskazini amekaribishwa kwa shangwe na umati wa watu waliokusanyika katika taifa hilo llilogawika juu ya utawala wa kifalme wa Uingereza. Mamia ya watu walijipanga barabarani kuelekea kwenye kasri ya Hillsborough, iliyo nje kidogo ya mji mkuu Belfast ambayo ni makazi rasmi ya familia ya kifalme katika Ireland ya Kaskazini.
Ingawa makaribisho ni mazuri huko Hillsborough, utawala wa kifalme wa Uingereza huvuta hisia mseto katika Ireland ya Kaskazini, ambako kuna jamuiya mbili kuu: wapo raia wengi wa nchi hiyo wanaoshiriki katika umoja wa Kiprotestanti na ambao wanajiona kuwa ni Waingereza na vilevile wapo waumini wa Kikatoliki wa kanisa la Roma wanaojiona kuwa wao ni Waairish. Mgawanyiko huo ulichochea ghasia kwa kipindi cha miongo mitatu kati ya makundi ya wanamgambo wa pande zote mbili na vikosi vya usalama vya Uingereza ambapo watu 3,600 walikufa.
Soma Zaidi: Mwili wa Malkia Elizabeth kupelekwa London
Wakati huo huo polisi wa Uingereza wamekosolewa na makundi ya kutetea haki na uhuru wa kijamii kuhusu jinsi wanavyowatendea waandamanaji wanaopinga utawala wa kifalme.
Kwingineko mamia ya watu waliupanga foleni kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Malkia Elizabeth wa pili hadi usiku wa manane wa kuamkia leo nje ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Giles katika mji wa Edinburgh, walipohudhuria mkesha wa kumuaga marehemu Malkia Elizabeth II.
Mfalme Charles wa tatu mwenyewe ameahidi kufuata nyayo za marehemu mama yake, Malkia Elizabeth wa pili kwa kuendeleza msingi wa amani katika Ireland ya Kaskazini. Alizungumza hay oleo Jumanne alipokutana na viongozi wa kisiasa wa Ireland Kaskazini, ikiwa ni pamoja na wale kutoka kwenye vyama vya kitaifa vinvyotaka Ireland Kaskazini ijiondoe kutoka Uingereza na kuwa sehemu ya Jamhuri ya Ireland.
Vyanzo:AFP/AP