1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Uingereza Charles lll aanza ziara nchini Ujerumani

29 Machi 2023

Mfalme wa Uingereza Charles lll na mkewe Camilla walitua katika uwanja wa ndege wa Berlin-Brundenburg, Jumatano. Wamekaribishwa na Rais wa Ujerumani Frank Walter- Steimeier na mkewe kwenye Lango la Brandenburg.

Deutschland | King Charles III besucht Berlin
Picha: WOLFGANG RATTAY/AFP

Mfalme wa Uingereza Charles III amewasili nchini Ujerumani kwa ziara yake ya kwanza ya kiserikali kama mfalme,  Ziara yake hiyo ni sehemu ya juhudi za kuwezesha kufunguliwa ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Uingereza na nchi za Umoja wa Ulaya baada ya nchi hiyo kuondoka kutoka kwenye jumuiya hiyo.

Mfalme wa Uingereza Charles lll na mkewe CamillaPicha: ODD ANDERSEN/AFP

Ndege ya familia ya kifalme, ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Berlin-Brandenburg muda mfupi kabla ya saa nane mchana kwa saa za Ulaya ya kati. Mfalme Charles wa tatu na mkewe Camilla walilakiwa kwa kupigwa milio 21 ya bunduki huku ndege mbili za kijeshi zikiruka juu kutoa heshima kwa wageni hao wa kifalme.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mkewe mama Elke Buedenbender waliwakaribisha wageni hao wa kifalme kwa dhifa ya kijeshi katika eneo la kihistoria la Lango la Brandenburg katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.

Mamia ya watu mashabiki wa familia ya kifalme ambao walianza kupanga foleni tangu asubuhi na mapema katika eneo hilo la Lango la Brandenburg wakitarajia kuwaona mfalme Charles lll na mkewe Camilla walisherehekea kuwaona mfalme Charles na mkewe Camilla. Mmoja wao ni Melanie Ames, mwenye umri wa miaka 33, na ameelezea furaha yake kwa kusema "Ni heshima kubwa kwa Ujerumani. Hakika ni ziara ya kwanza ya kiserikali ya Mfalme Charles wa tatu tangu awe mfalme. Ingawa bado hajatawazwa lakini ziara yake hapa Ujerumani ni ziara maalum sana."

Picha ya pamoja ya Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier, Mfalme Charles lll na wake zao kwenye eneo la kihistoria la Lango la Brandenburg.Picha: Getty Images

Mfalme Charles wa tatu mwenye umri wa miaka 74, alipanda kwenye kiti cha enzi baada ya kifo cha mama yake Malkia Elizabeth II mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita. Anatarajiwa kutawazwa mnamo tarehe 6 mwezi Mei mwaka huu.

Awali alikuwa amepanga kuzuru kwanza nchini Ufaransa lakini aliahirisha safari yake kwa sababu ya maandamano makubwa ya kupinga mabadiliko katika mfumo wa pensheni nchini humo.

Siku ya Alhamisi, mfalme Charles lll atatoa hotuba kwenye Bunge la Ujerumani. Pia atakutana na Kansela Olaf Scholz, baadae atakutana na kuzungumza na wakimbizi wa Ukraine, na kisha atakutana na wanajeshi wa Uingereza na Ujerumani wanaofanya kazi katika miradi ya pamoja. Mchana kesho atatembelea shamba linaloendesha kilimo kwa kutumia mfumo wa udhibiti wa wadudu unaozingatia ikolojia na mbolea za kibaiolojia zinazotokana kwa na taka za wanyama na mimea lililopo nje ya jiji la Berlin.

Mamia ya watu waliofurika kumlaki Mfalme Charles lll na mkewe Camilla katika Lango la Brundenburg.Picha: Michelle Tantussi/REUTERS

Ziara ya Mfalme Charles na mkewe Camilla itawapeleka katika jiji la Hamburg siku ya Ijumaa, ambapo watatembelea jumba la kumbukumbu la Kindertransport, kwa watoto wa Kiyahudi waliokimbia kutoka Ujerumani kwenda Uingereza wakati wa Utawala wa Manazi kuanzia mwaka 1871 hadi mwaka 1918. Vilevile atawakumbuka wahasiriwa wa shambulio la anga la mwaka 1943 katika jiji hilo. Baada ya hapo katika siku hiyo hiyo ya Ijumaa atahudhuria hafla kuhusu nishati mbadala kabla ya kuanza safari ya kurudi Uingereza. Mfalme Charles wa tatu, kwa miongo kadhaa amekuwa anahamasisha ajenda ya mazingira.

Ndege iliyomleta Mfalme Charles lll nchini UjerumaniPicha: ODD ANDERSEN/AFP

Kulingana na taarifa za Kasri la Buckingham mfalme Charlles wa tatu atashughulikia maswala yanayozikabili nchi zote mbili za Ujerumani na Uingereza kama maswala ya uendelevu katika maswala mbalimbali na mgogoro wa Ukraine.

Vyanzo: DPA/AP/AFP