1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfanyabiashara tajiri Tanzania Mohamed Dewji atekwa

Hawa Bihoga11 Oktoba 2018

Jeshi la polisi nchini Tanzania limethibitisha kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewj. Watu watatu wamekamatwa kwa uchunguzi zaidi

Tansania Kidnapping Mohamed Dewj
Picha: DW/S. Khamis

Mfanyabiashara mashuhuri barani Afrika mwenye maskani yake jijini Dar es Salaam Mohamed Dewj ametekwa nyara na watu wasiojulikana alfajiri ya leo. Jeshi la polisi nchini humo limethibitisha kutekwa kwa mfanyabiashara huyo na mwekezaji wa timu kongwe ya soka, Simba na kuongeza kuwa watu watatu wametiwa mbaroni kwa uchunguzi zaidi.

Mapema leo asubuhi katika hoteli ya Colosseum hali ya sintofahamu iliwashangaza na kuwapa hofu Wateja na hata walio karibu na hoteli hiyo baada ya kusikika milio ya risasi ambayo haikufahamika kwa haraka nani aliyeifyatua risasi hizo.

Lakini baada ya Sekunde kadhaa ndipo watu waliokuwa katika hoteli hiyo wakashuhudia mfanyabiashara na bilionea mkubwa Afrika Mohammed Deuwj akichukuluwa kwa nguvu kutoka kwenye gari aina ya Range Rover na kuingizwa kwenye gari aina ya safu ambapo liliondoka kwa mwendo wa kasi likielekea kusiko julikana ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa walikuwemo miongoni mwa wengine wanaume wawili wenye asili ya kizungu.


Polisi yaendelea na uchunguzi

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Dar es Salaam na pia Mkuu wa mkoa Paul Makonda asema vyombo vya ulinzi vinaendelea na michakato ya kuwatafuta wahalifu waliomteka mfanyabiashara huyo.Picha: DW/S. Khamis

Katika kupata uhakika wa Jambo hili, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa amewaambia waandishi habari, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ambapo hadi sasa watu watatu wameshikiliwa.

Katika hili onyo Kali likatolewa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kutumia tukio hilo katika nyanja za kisiasa na hata watakaochapisha taarifa zisizo za kweli kwenye mitandao ya kijamii Kuhusu tukio hilo watachukuliwa hatua na mamlaka husika.

Watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara wasanii na Jamii kwa ujumla wamechapisha habari hiyo kwenye mitandao ya kijamii huku wakionyesha masikitiko makubwa kutokana na tukio hilo wanalosema halivumiliki.

Msemaji wa klabu ya simba Haji Manara akizungumza na wanahabari amewataka wanasimba kutulia na kuwa wavumilivu wakati vyombo vya usalama vikiendelea kuchunguza zaidi.

Tukio hilo la utekwaji nyara mfanyabiashara huyo mashuhuri barani Africa ni miongoni mwa matukio ya utekaji yanayoelezwa kwamba yanafanywa na watu wasiojulikana nchini Tanzania.

Mhariri:Yusuf Saumu