1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, mfuko wa dharura EU umeshindwa kuhudumia wahamiaji?

Hawa Bihoga
26 Septemba 2024

Wakaguzi wa hesabu wanasema mfuko wa euro bilioni 5 wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Afrika hautoshi kushughulikia uhamiaji, kiasi kwamba, hatari dhidi ya haki za binadamu hazikushughulikiwa ipasavyo.

Mpaka baina ya nchi na nchi
Mpaka baina ya nchi na nchiPicha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Katika ripoti iliyozusha mshtuko mkubwa, Mahakama ya Wakaguzi wa Hesabu ya Ulaya, ECA, ilisema Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Ulaya wa Euro bilioni 5 kwa ajili ya Afrika, EUTF, unashindwa kushughulikia ipasavyo suala la uhamiaji, kwa sababu unatumika pia kufadhili mambo mengine kadhaa katika sekta za maendeleo, msaada wa kibinadamu na usalama.

Mfuko huo ulianzishwa wakati wa kilele cha mzozo wa wakimbizi wa mwaka 2015 na unalenga kushughulikia sababu kuu za ukosefu wa utulivu, uhamiaji usiofuata sheria na watu walioyakimbia makaazi yao barani Afrika.

Lakini mwaka mmoja kabla ya kumalizika kwa mpango huo, wakaguzi walisema haukujikita vya kutosha juu ya vipaumbele vya kushughulikia mizizi ya uhamiaji.

Soma pia:Jeshi la wanamaji la Senegal laopoa miili 30 iliyokuwa karibu na pwani ya Senegal

Ripoti hiyo inasema malengo ya vipaumbele vya mpango huo vilitanuliwa kadiri iwezekanavyo, ili kuzingatia hatua nyingi zaidi, lakini baadhi ya miradi iliyofadhiliwa inaonekana kuwa na uhusiano kidogo mno na uhamiaji, kama vile ukarabati wa jumba la maonyesho la Kirumi nchini Libya au kituo cha redio huko Sahel.

Katika ugunduzi muhimu wakaguzi walisema ufadhili huo haukuwa na msingi wa viashiria maalum vya uhamiaji kama vile idadi ya wahamiaji haramu wanaowasili katika Umoja wa Ulaya, uundaji wa nafasi za kazi uliongezwa kupita kiasi, na hatari za haki za binadamu hazikushughulikiwa ipasavyo.

Zaidi ya hayo, katika baadhi ya matukio kulikuwa na hatari kwamba mapato yaliyoongezeka yangeliweza kuwa na athari ya kinyume ya kuchochea uhamaji zaidi badala ya kuudhibiti.

Wakaguzi: Mfuko ulikuwa na mafanikio kiasi

Bettina Jakobsen, Mjumbe wa ECA anayehusika na ukaguzi huo, aliongeza kuwa ingawa EUTF ilisaidia kuweka uhamiaji juu katika ajenda ya maendeleo na kisiasa, kulikuwa na mabadiliko kidogo katika lengo la mfuko huo, ambalo linabaki kuwa pana sana, licha ya ugunduzi kama huo katika ripoti ya mwisho mwaka 2018.

Walinzi wa mpakani wakifanya ukaguzi Uhispania.Picha: Antonio Sempere/Europa Press/IMAGO

Mpango wa EUTF ulizinduliwa baada ya kuzuka kwa vita vya Syria na wimbi la wakimbizi mwaka huo. Lakini wataalam wanaamini kuwa ulikuwa na wigo mpana wa kijiografia na ufadhili wake ulitolewa kwa kulingana na hali inayojitokeza.

Mfuko huo ulishughulikia mizozo katika kanda tatu kubwa, Sahel na Ziwa Chad, Pembe ya Afrika na Afrika Kaskazini, na uliyasaidia mataifa 27 kwa mikataba 933 chini ya programu 248.

Soma pia:Uholanzi inataka kujiondoa katika kanuni za uhamiaji za Ulaya

Ufadhili huo uligawanywa kupitia miradi mbalimbali katika maeneo manne muhimu. Fursa kubwa za kiuchumi na ajira zilitengewa asilimia 17 ya ufadhili, asilimia 28 kwa ajili ya kuimarisha ustahimilivu wa jamii, asilimia 31 kwa usimamizi bora wa uhamiaji na asilimia 22 kwa ajili ya uboreshaji wa utawala na kuzuia migogoro.

Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha kuwa hakuna mwongozo wowote kuhusu ni kipi kati ya vipaumbele hivi kinapaswa kuzingatiwa zaidi. Licha ya hayo, ripoti iligundua kuwa uundaji wa ajira uliongezwa kupita kiasi na katika matukio kadhaa ulibainika kutokuwa endelevu.

Wakaguzi waligundua mifano ya kuripoti kupita kiasi na uwasilishaji potofu wa idadi ya maeneo ya viwanda na miundombinu ya biashara. Walisema miradi minne katika sampuli yao iliripoti jumla ya maeneo ya viwanda na miundombinu 62 ya biashara iliyojengwa, kupanuliwa au kuboreshwa.

Lakini hawakuweza kupata taarifa za kutosha kuthibitisha uwepo wa karibu nusu ya miradi iliyoripotiwa. Walisema katika miradi mingine, idadi ya nafasi za ajira ilizidishwa.

Ethiopia ilinufaika na mfuko wa EU

Nchini Ethiopia kwa mfano, ripoti ilisema mradi wa kuzuwia uhamiaji haramu kwa kuimarisha ajira, ulipunguza ukosefu wa ajira katika maeneo matano ya uhamiaji kwa asilimia 0.32 tu, na kufikia asilimia 3.61 ya lengo lililowekwa.

Niels Keijzer, Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Maendeleo na Uendelevu ya Ujerumani, aliiambia DW kuwa mfuko huo wa Umoja wa Ulaya ulikuwa na utata tangu mwanzo, kwa mfano, kwa sababu baadhi ya nchi wanachama zilitanguliza matumizi katika miradi ya kufanya mipaka kuwa migumu kupitia ufadhili wa mataifa ya ulimwengu wa tatu na mashirika yao ya usimamizi wa sheria.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

01:56

This browser does not support the video element.

Soma pia:Ujerumani yatanua ukaguzi mipakani kudhibiti wahamiaji

Wengine walionya mapema mwaka 2017 kuhusu mwelekeo mpana wa kuufanya msaada wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya kuwa salama.

Kutokana na hatari kubwa ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Libya, ripoti hiyo inasema Umoja wa Ulaya ulianzisha ufuatiliaji wa kwanza wa aina yake wa upande wa tatu wa haki za binadamu.

Lakini halmashauri kuu ilikosa utaratibu rasmi wa kuripoti, kurekodi na kufuatilia madai ya ukiukaji wa haki kuhusiana na miradi ya Umoja wa Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW