1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaSudan Kusini

Mfumo wa afya Sudan Kusini uko taabani

9 Machi 2026

Mfumo wa afya nchini nchini Sudan Kusini umeparaganyika kutokana na rushwa ya miaka mingi hali inayofanya viongozi kukimbilia nchi jirani ili kutibiwa.

Sudan Kusini Juba 2018 | Mama akiwa amemshika mtoto wake mchanga mikononi mwake katika Hospitali ya Mafunzo ya Juba
Sekta ya tiba nchini Sudan Kusini inakabiliwa na changamoto kubwa na hasa kutokana na tatizo la rushwa iliyokithiriPicha: Stefanie Glinski/AFP/Getty Images

Hali kwenye sekta ya kiafya imefikia pabaya kiasi kwamba hivi karibuni gavana wa jimbo moja la Sudan Kusini alilazimika kusafiri kwenda nchi jirani ya Kenya ili kupata matibabu ya shinikizo la damu. Lakini si wote nchini humo wanaweza kupata urahisi wa aina hiyo.

Riek Gai Kok ni gavana wa jimbo la Jonglei, eneo ambako makabiliano kati ya serikali na upinzani wa Sudan Kusini yameanza tena.

Hivi karibuni alisafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kupatiwa matibabu. Wale wanaotoa msaada wa kiutu nchini Sudan Kusini wanalitaja suala hilo kuwa mfano wa jinsi tabaka tawala lililovyoruhusu huduma za kijamii kusambaratika, pengine kwa sababu wana hakika ya kuzipata mahala pengine.

Sudan Kusini inaorodheshwa na shirika la Transparency International kuwa miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu vya rushwa.

Vita vipya vya kiraia vyaizorotesha zaidi sekta ya afya

Katika wakati nchi hiyo imetumbukia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya pande hasimu, huduma za afya zilizobakia zinatokana na ufadhili wa kigeni kupitia mashirika ya Msalaba Mwekundu na Madaktari Wasio na Mipaka.

Shirika la Habari la AFP liliitembelea hospitali kwenye mji mkuu Juba walikutana na askari mmoja ambaye alishangaa alipopatiwa msaada wa kusafirishwa kwa ndege kwenda hospitali katika nchi ambayo wengi ya wanaojeruhiwa kwenye mzozo hutelekezwa na kufa.

Mwanajeshi wa SPLA-IO akiwa na silaha mbele ya majengo ya serikali huko JongleiPicha: Luis Tato/AFP

"Nilipopigwa risasi, nilijua nimekufa," anasema mwanajeshi huyo Ajuong Deng, aliyejeruhiwa mguuni. Lakini ilikuwa ni Shirika la Msalaba Mwekundu ndiyo lilimsaidia. Siyo serikali wala jeshi analolitumikia.

Kwenye hospitali hiyo, matabibu wanaosadiwa kifedha na mashirika ya hisanikutokana na mishahara yao kuchelewa kwa miezi mingi, wanatiwa na wasiwasi na athari za kiafya kutokana na mzozo unaoendelea.

Katika nchi ambayo kilometa 300 pekee za barabara ndiyo zimetiwa lami, na nyingi hazipitiki wakati wa mvua, wengi wanaojeruhiwa huishia kupata maambukizi kabla hata ya kufika hospitali. Daktari wa tiba ya viungo kutokana Shirika la Msalaba Mwekundu anayehudumu kwenye hospitali ya mjini Juba, Angeth Jervas Majok anasema wengi yao huishia kukatwa viungo.

Hadi sasa serikali ya Sudan Kusini haijasema ni wanajeshi wangapi wameuawa tangu mapigano yalipochacha mwaka uliopita.

UN: Maelfu ya watu wameuawa na wengine wayakimbia makazi yao

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya raia 5,100 wameuawa na mamia kwa maelfu wamepoteza makaazi yao, na umetahadharisha Sudan Kusini imo kwenye ukingo wa kutumbukia kwenye, "vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe".

Maisha ya wakimbizi katika kambi ya Thobo nchini Sudan

02:03

This browser does not support the video element.

Vita vya mwisho vya miaka ya 2010 vilisababisha vifo vya watu 400,000.

Licha ya utajiri mkuu wa mafuta unaiingizia nchi hiyo zaidi ya dola bilioni 25 kila mwaka tangu 2011, ni asilimia moja tu ya bajeti ya mwaka huu imetengwa kwa ajili ya afya. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema zaidi ya asilimia 92 ya umma wa nchi hiyo unaishi kwenye umasikini wa kupindukia,

Usalama pia ni mdogo kiasi wafanyakazi wa mashirika kama Msalaba Mwekundu na Madaktari Wasio na Mipaka wanahofia maisha yao. Vituo vyao vimeshambuliwa mara kumi na moja mwaka uliopita.     

Marekani tayari imeonya itaondoa ufadhili wake ikiwa hali haitoimarika na taasisi za hisani zimeanza kupunguza misaada yao kutokana na kuvunjwa na viongozi wa nchi hiyo.

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny alipoulizwa na AFP amesema kuna hali ngumu ya kifedha na serikali inajitahidi kutafuta njia ya kusuluhisha hali hiyo. Lakini bila kupambana kikamilifu na rushwa, Sudan Kusini itaendelea kukabiliwa na matatizo yasiyo na kikomo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW