Mfumo wa Elimu katika baadhi ya majimbo ya Uhispania,wabagua wageni.
11 Novemba 2004Malalamiko yamepamba moto nchini Spain, juu ya mfumo wa elimu katika majimbo mawili ya nchi hiyo, unaozuia wageni kuendelea na masomo, baada ya darasa la kumi.
Watetezi wa haki za binaadamu, waalimu, na wanasiasa wa vyama vya kisiasa vya mrengo wa kushoto, wanalalamika dhidi ya kile wanachokielezea kuwa aibu kubwa, enzi hizi, kuwa nchi mwanachama wa Jumuia ya Umoja wa ulaya, inaweza kuwa na mfumo wa elimu unaobagua wageni. Majimbo hayo mawili yanayohusika, yanaelezewa kuwa shina la wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia.Ukweli ni kuwa serikali za majimbo hayo zinadhibitiwa na vyama vya mrengo wa kulia.
Inasemekana kuwa mfumo huo unalenga kuwabagua hasa watoto wenye asili ya afrika ya kaskazini-Wahamiaji kutoka nchi kama vile Morocco, Tunisia, Algeria na Mauritania, ni wengi nchini Spain, na wameanza kuwasili katika nchi hiyo, tangu karne iliyopita-
Mwanasiasa mmoja wa chama cha kisoshalisti, kinachoiongoza spain wakati huu, amenukuliwa na shirika la habari IPS, akisema kwamba ni aibu kubwa, kwamba nchi kama spain yenye historia ya kukaribisha wageni na kuheshimu haki za binadamu hususan wanyonge, inavumilia mfumo wa ubaguzi katika baadhi ya majimbo yake. Amesema ni jambo lisiloingia akilini, kwamba mnamo wakati ambako dunia nzima inajaribu kupiga hatua katika kuimarisha usawa na hasa kuhakikisha haki za waliowachache zinaheshimiwa, nchini Spain watoto wa wahamiaji wanakataliwa elimu, jambo ambalo matokeo yake ni kuwatenga watoto hao katika maendeleo jumla ya jamii-
Majimbo ya Madrid na Valencia, yanayodhibitiwa na vyama vya mrengo wa kulia, yamepitisha sheria inayowakatalia watoto wa wahamiaji ambao hawajakuwa na vibali rasmi vinavyowaruhusu kuishi spain kwa mda mrefu, kuendelea na elimu yao baada ya kidato cha nne; yaani mwaka wa kumi wa masomo.
Uamuzi huo ni kinyume kabisa, wanasema wanasiasa wa vyama vya kisoshalisti, na haki ya elimu kwa kila binaadamu, bila kujali anakotokea, rangi yake ya mwili, dini, au sababu nyingine zinazotumiwa kubagua watu. Wanasema kwamba mnamo wakati ambako kutompeleka mtoto shule kunaweza kusababisha adhabu kwa raia yeyote wa spain na mgeni anaeishi katika nchi hiyo, uamuzi uliochukuliwa na serikali za majimbo hayo hauwezi kueleweka.
Matokeo ya watoto wa wageni kutokubaliwa kuendelea na elimu yao zaidi ya miaka kumi, ni kuwa hawawezi kupata vyeti vinavyotolewa na vyuo vikuu, na hivyo hawatakuwa na uwezo sawa na wa wenzao raia wa spain, wa kushindana katika masoko ya kazi.
Kwa mujibu wa shirika moja lisilokuwa la kiserikali, linalotetea haki za wageni nchini Spain, wakati huu jumla ya wanafunzi laki moja, hawawezi kuendelea na elimu, kutokana na uamuzi huo wa jimbo la Madrid na la Valencia, kwa kuwa hawana nyaraka za uhamiaji zinazohitajika.
Kulingana na ripoti ya shirika hilo, katika mji mkuu wa Spain Madrid peke yake, wanafunzi zaidi ya elfu tatu mianane, wamelazimika kusimamisha elimu, kutokana na uamuzi huo wa viongozi wa jimbo la Madrid.
Jimbo la Madrid na la Valencia, majimbo hayo mawili, miongoni mwa majimbo kumi na saba ya taifa la Spain, ndiyo yenye kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji, wengi wao wakiwa kutoka nchi za Afrika ya kaskazini na mataifa ya Amerika ya kati, makoloni ya zamani ya Spain. Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa mjini Madrid peke yake, wanaishi wageni zaidi ya laki tano na themanini elfu. Shida iliyopo ni kuwa, karibu nusu ya watu hao, hawana vyeti vinavyowaruhusu kuishi nchini Spain.Wenyewe viongozi wa majimbo hayo, hawaoni uamuzi walioupitisha kama kikwazo dhidi ya baadhi ya wanafunzi wa kigeni kuwa na elimu ya juu, wala hawakubaliani na maoni ya wale wanaochukulia mfumo wa elimu katika majimbo hayo kuwa ni wa ubaguzi.
Afisa mmoja wa utawala katika jimbo la Valencia, ameliambia shirika la habari kuwa malalamiko ya aina hiyo ni upuuzi mtupu. Akasema serikali za majimbo hayo zinahofanya ni kuheshimu sheria, kwa kuchukua hatua zinazolazimisha wageni kuwa na nyaraka zinazohitajika ili waishi nchini Spain.Amesema jimbo lake haliwakatalii wanafunzi kuendelea na elimu kwa misingi ya kule wanakotokea. Akasema sheria kuhusu kupewa au kutopewa kibali cha kuishi Spain zinatungwa na serikali kuu, kwa hiyo serikali hiyo ndiyo inayostahiki kutatua swali hilo, ili waliokubaliwa kuishi nchini Spain waweze kufaidika na huduma zote zinazotolewa na nchi hiyo.Kwa vyovyote vile, watetezi wa haki za binaadamu wanasisitiza kuwa, sheria inatumiwa kutenda haki, lakini inaweza kutumiwa pia kudhulumu-