Mfumo wa elimu nchini Afrika Kusini wakabiliwa na matatizo
31 Januari 2008Walimu ambao hawajapokea mafunzo mazuri, migomo ya walimu na ugonjwa wa ukimwi, ni mambo yanayouathiri sana mfumo wa elimu nchini Afrika Kusini.
Maelfu ya wanafunzi huacha masomo bila kuwa na ujuzi msingi wa kuwawezesha kuendelea na masomo ya juu au kupata kazi zinazohitaji ujuzi wa mikono.
´Ikiwa tutaupa kipau mbele mfumo wa elimu, pengine tutakuwa tunaanza kulishughulikia tatizo lililopo, amesema Graeme Bloch, mtaalamu wa elimu katika benki ya maendeleo ya Afrika Kusini.
Kuhusu swali ikiwa sera tofauti za elimu katika mikoa mbalimbali nchini nchini Afrika Kusini zinasaidia kuyafikia malengo ya elimu, Bloch amesema anaamini nchi inahitaji udhibiti mkubwa zaidi wa kitaifa.
Idara ya kitaifa ya elimu haipaswi peke yake kuwa taasisi inayounda sera. Inapaswa kuwepo wizara moja ya elimu lakini pia kuwe na nafasi ya mipango maalumu ya mikoa.
Umaskini mara kwa mara unalaumiwa kwa matokeo mabaya ingawa shule kadhaa katika maeneo ya mashambani hupata matokeo mazuri katika mitihani.
Ufanisi unategemea sana kiongozi wa shule. Kuna mwalimu mkuu ambaye huileta jamii katika shule. Ana wanachama wa jamii hiyo wanaohusika katika miradi inayosaidia kupata fedha kwa ajili ya matumizi ya shule na jamii. Mwalimu huyu mkuu amejipanga sio tu kuinufaisha jamii pekee lakini pia hata shule.
Matatizo yanayozikabili shule katika mikoa mbalimbali yanadhihirika katika matokeo ya mitihani. Katika majimbo ya KwaZulu Natal, Mpumalanga, Limpopo na Eastern Cape, matokeo ni mabaya mno.
Majimbo yaliyo katikati ni pamoja na jimbo la Kaskazini magharibi na Free State huku matokeo mazuri yakionekana katika majimbo ya Gauteng, Northern Cape na Western Cape.
Lawama zote hazipaswi kutupiwa idara za elimu kwa matokeo mabaya ya mwisho wa mwaka. Mwaka jana walimu walifanya mgomo nchini kote kwa mwezi mmoja. Walioathirika kutokana na mgomo huo ni wanafunzi.
Tatizo la elimu linaweza kutatuliwa ikiwa jamii yote itaiunga mkono wizara ya elimu. Walimu wanapaswa wasaidiwe na serikali. Wapewe vitabu vya kufundishia na vifaa vyengine vinavyohitajika kwa mafunzo. Na vitu hivi vyote vinatakiwa viwepo wakati shule zinapofunguliwa mwanzoni mwa kila mwaka.
Kuna tatizo kubwa la upungufu wa walimu waliosomea kazi ya ualimu. Mfumo wa elimu unaozingatia matokeo uitwao ´Outcomes Based Education´ OBE, kwa kifupi, umekosolewa. ´Ipo haja ya kudurusu njia za kuwapa mafunzo walimu,´ amesema Graeme Bloch.
Mfumo wa OBE hauwezi kutekelezwa nchini Afrika Kusini kwa kuwa unategemea sana juhudi na bidii za mwanafunzi na ushirikiano kati ya mwalimu na mwanafunzi uwe mzuri sana. Mfumo huo unaweza tu kutekelezwa katika mazingira ambayo walimu wanasaidiwa vizuri, jambo ambalo halipo nchini Afrika Kusini.
Mfumo wa OBE unalenga kumfanya mwanafunzi afikirie mambo kwa kina na unataka mwanafunzi ajifanyie kazi zake mwenyewe. Ni vigumu kuutekeleza mfumo huo katika eneo ambalo halina vitabu, mashine za kupiga chapa, maktaba au vifaa vyengine vya kusaidia mchakato wa kufundisha.
Kasi ya watoto kuacha masomo yao nchini Afrika Kusini ni kubwa. Graeme Bloch wa benki ya maendeleo ya Afrika Kusini anasema ni vigumu kulitatua tatizo hili katika nchi ambamo watoto wanalazimika kuvuka mito iliyofurika, ambako hakuna mifumo ya usafiri, wanafunzi wanakwenda shule wakiwa na njaa na ambamo wengi wana jukumu la kuziongoza familia zao baada ya kuwapoteza wazazi wao kutokana na ugonjwa wa ukimwi.
Pia kuna tatizo la lugha. Imegunduliwa kwamba wanafunzi wanaofundishwa kutumia lugha ya mama hufanya vizuri shuleni. Serikali imeanza kutengeneza vifaa katika lugha mbalimbali. Hata hivyo tatizo ni kwamba walimu wenyewe huenda pengine wasiifahamu lugha ya mama barabara.
Wanafunzi katika maeneo yaliyo maskini wanasamehewa kulipa karo ya shule. Hata hivyo mfumo huu unatekelezwa kwa awamu na huenda uchukue muda mrefu kabla kuwanufaisha watoto wote maskini. Pia kumekuwa na malalamiko nchini Afrika Kusini kwamba elimu ya bure inaigharibu serikali fedha nyingi.
Graeme Bloch anasema ipo haja ya wadau wote kushirikiana ili kuyatatua matatizo yanayoukabili mfumo wa elimu nchini Afrika Kusini.