1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfumo wa Pamoja wa Hifadhi EU waleta hofu kwa waomba hifadhi

Iddi Ssessanga /Marcel Fürstenau
3 Juni 2026

Wakati EU ikijiandaa kuanza kutekeleza mfumo mpya wa pamoja wa kudhibiti utoaji hifadhi na uhamiaji, wataalamu waonya hatua hizo huenda zikaongeza ugumu kwa watu wanaotafuta hifadhi badala ya kutatua tatizo la msingi.

Türkei Suruç 2014 | Syrische Flüchtlinge fliehen vor dem IS aus Kobani
Wataalamu wa masuala ya uhamiaji wana wasiwasi kuhusu Mfumo wa Pamoja wa Hifadhi wa Umoja wa Ulaya, unaotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuniPicha: Burhan Ozbilici/AP Photo/picture alliance

Wataalamu wa masuala ya uhamiaji nchini Ujerumani wana wasiwasi kuhusu Mfumo wa Pamoja wa Hifadhi wa Umoja wa Ulaya, unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi huu. Kwa mujibu wa Petra Bendel kutoka Chuo Kikuu cha Er-langen-Nürnberg, mfumo huo unaweza kusababisha ongezeko la vituo vya kuwahifadhi waomba hifadhi katika mazingira yanayofanana na kizuizini kwenye mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya.

Mojawapo ya vipengele vinavyosababisha mjadala ni  mpango wa kuanzisha vituo vya kurejesha wahamiaji  nje ya Umoja wa Ulaya, maarufu kama "Return Hubs.” Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobri-ndt, ameutetea mpango huo kama suluhisho la ubunifu. Hata hivyo, wakosoaji wanaonya kuwa unaweza kuathiri haki za watu wanaotafuta hifadhi.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, makundi yaliyo katika mazingira hatarishi zaidi, yakiwemo wanawake, watoto na familia zinazokimbia migogoro, yanaweza kuathiriwa zaidi. Pia wamekosoa uamuzi wa serikali ya Ujerumani kusitisha baadhi ya programu za kuwahamisha watu walio hatarini kutoka Afghanistan, wakisema hatua hiyo inapunguza wajibu wa nchi kutoa ulinzi kwa wanaouhitaji.

Idadi ya waomba hifadhi Ujerumani yapungungua

Licha ya mjadala mkali wa kisiasa kuhusu uhamiaji, takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya waomba hifadhi nchini Ujerumani imepungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa kiwango cha dunia, zaidi ya watu milioni 117 wako katika hali ya ukimbizi au wamehamishwa makwao.Picha: Marcel Beloqui Evardone/SIPA/picture alliance

Mwaka 2023 zaidi ya watu 330,000 waliwasilisha maombi ya hifadhi kwa mara ya kwanza. Miaka miwili baadaye idadi hiyo ilishuka hadi takribani watu 113,000. Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, maombi yalikuwa karibu 22,000 pekee.

Kwa kiwango cha dunia,  zaidi ya watu milioni 117 wako katika hali ya ukimbizi au wamehamishwa makwao. Hiyo ni karibu mara mbili ya idadi iliyokuwepo muongo mmoja uliopita. Wengi wao ni wakimbizi wa ndani wanaokimbia vita, ukame, mafuriko na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi, na kati yao ni sehemu ndogo tu inayofika Ulaya au Amerika Kaskazini.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa katika baadhi ya maeneo watu wameanza kurejea makwao. Nchini  Ukraine,  ambako vita dhidi ya Urusi vinaendelea, takribani watu milioni nne wamerudi katika miji na vijiji vyao. Hata hivyo, wataalamu wanasema hali ni tofauti kabisa nchini Syria ambako uharibifu wa miundombinu, umaskini mkubwa na ukosefu wa usalama bado vinazuia kurejea kwa wakimbizi kwa kiwango kikubwa.

Waandishi wa ripoti hiyo wanaonya pia kuhusu kupungua kwa misaada ya kibinadamu na fedha za maendeleo kutoka kwa nchi wafadhili. Wanasema ikiwa jumuiya ya kimataifa itaendelea kupunguza msaada kwa wakimbizi na nchi zinazokumbwa na migogoro, sababu zinazo walazimu watu kukimbia makwao zitaendelea kuongezeka. Kwao, suluhisho la muda mrefu si kujenga vizuizi vipya, bali kuwekeza zaidi katika amani, maendeleo na ulinzi wa watu walio hatarini.

Ugumu wa maisha ya waomba hifadhi Ubelgiji

00:55

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW