1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Mwaka wa kwanza mgumu kwa Ruto madarakani

13 Septemba 2023

Gharama za chakula na kodi ziko juu, upinzani ni mkali na Wakenya wamekasirika. Rais William Ruto amepoteza uugwaji mkono mkubwa nyumbani. Ni wakati wake wa kuwasikiliza waliompigia kura, baadhi ya wataalam wanasema.

Rais wa Kenya William Ruto
Rais William Ruto ametimiza mwaka mmoja madarakani akikabiliwa na changamoto chungumzima.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Rafu zimejaa katika duka la Anita Wairimu katikati mwa jiji la Nairobi, lakini hakuna kinachouzwa. Hakuna mtu aliye na pesa za ziada, alielezea, wateja wake wanapambana kukidhi mahitaji.

"Nimekuwa na duka hili kwa miaka minane. Huu umekuwa mwaka mgumu zaidi. Ni mbaya zaidi kuliko wakati wa Covid," mama huyo asiye na mume mwenye umri wa miaka 44 aliiambia AFP.

Wairimu analaumu masaibu yake kwa mwanamume ambaye alimpigia kura rais kwa shauku -- William Ruto, ambaye aliingia madarakani mwaka mmoja uliopita akiahidi kufufua uchumi uliokumbwa na msukosuko na kuleta ustawi kwa "wapambanaji" wa Kenya wanaofanya kazi kwa bidii.

Ruto alishinda kwa kura chache katika uchaguzi wa Agosti 2022 kufuatua kampeni yake iliyoahidi mpango wa kukuza uchumi kuanzia "chini" na kuweka fedha zaidi mifukoni mwa wafanyabiashara wadogo, wafanyakazi wasio rasmi, na wengine wanaotafuta riziki ya kila siku.

Lakini badala yake, alianzisha kodi mpya, na bei kwa Wakenya wa kawaida zimepindukia.

Je, maandamano ndio suluhu ya matatizo yanayoizonga nchi?

03:16

This browser does not support the video element.

Mfumuko wa bei ulishuka hadi asilimia 6.7 mwezi Agosti lakini katika mwaka uliopita bei ya petroli imeongezeka kwa asilimia 22, umeme kwa karibu asilimia 50, na bidhaa kuu za kaya kama sukari na maharage kwa asilimia 61 na asilimia 30 mtawalia.

Soma pia: Rais William Ruto atimiza mwaka mmoja madarakani

Kenya ambayo ndiyo kitovu cha biashara Afrika Mashariki, haikunusurika na mlipuko wa janga la Covid-19 na vita nchini Ukraine ambavyo vilileta maumivu kwa uchumi kote ulimwenguni, na ufufukaji wake ulizuiwa pia na ukame uliovunja rekodi.

Wafuasi wa Ruto wavunjwa moyo

"Uchumi ni mbaya kila mahali duniani, ni tatizo la kimataifa," alisema Simon Migwi, dereva wa teksi ya pikipiki mwenye umri wa miaka 40 aliye tayari kumpa Ruto nafasi nyingine.

Lakini baadhi ya matatizo ni ya kujitakia mwenyewe, wadadisi walisema, imani ambayo imeshika hatamu miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa Ruto.

"Nilifurahi sana alipoapishwa... sasa nimesikitishwa sana," Wairimu aliiambia AFP, akisema mapato yake ya kila siku ya takriban shilingi 1,000 za Kenya (dola 6.8) yalikuwa yamepungua kwa nusu tangu Ruto aingie madarakani. "Ni sisi, wapambanaji, ambao tunateseka zaidi."

Uchumi wa Kenya umekumbwa na deni la dola bilioni 69 na shilingi imepoteza asilimia 30 ya thamani yake dhidi ya dola katika kipindi cha miezi 18. Mambo haya yamesababisha ukuaji wa uchumi, ambao unatabiriwa mwaka 2023 kuwa chini kuliko asilimia 4.8 iliyorekodiwa mwaka jana.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amekuwa mwiba mchungu aktika utawala wa Ruto.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Ken Gichinga, mwanauchumi mkuu katika kampuni ya uchanganuzi ya Mentoria Economics, ameuelezea mwaka wa kwanza wa Ruto kama "kipindi chenye changamoto nyingi".   "La kwanza, mazingira ya kimataifa si rahisi. Na la pili, sera zilizowekwa hazijafanya kazi." 

"Hustler fund" au mfumo wa wapambanaji wa Ruto, ambayo ni sera kuu ya utoaji mikopo midogo midogo kusaidia Wakenya wasio na pesa kuanzisha biashara na kuchochea uchumi, pia haikufanya kazi kama ilivyokusudiwa, alisema.

Sikiliza mahojiano: 

Rais William Ruto atimiza mwaka mmoja madarakani.

This browser does not support the audio element.

Kuanzishwa kwa msururu wa ushuru mpya -- hasa kuongezeka maradufu kwa VAT kwenye nishati ya mafuta -- kulipunguza uwezo wa ununuzi zaidi.

Serikali ilisema uchungu huo ulikuwa muhimu ili kuondoa uchafu ulioachwa na utawala uliopita -- ambamo Ruto alihudumu kama naibu rais kwa muongo mmoja.

Kupanda kwa kodi na kupunguzwa kwa ruzuku ya mafuta na chakula kulikaribishwa kwa mapana na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, na Benki ya Dunia, ambayo yalitoa mikopo kama jibu.

Lakini mitaani, mapokezi yamekuwa ya baridi    

"Waliwadanganya wafanyabiashara, waliwalaghai ma hustler," alisema Robert Kiberenge, mwanamume mwenye umri wa miaka 47 ambaye hana kazi kwa muda mrefu.  

Kiberenge alimpigia kura Raila Odinga -- kiongozi mkongwe wa upinzani ambaye bado anadai uchaguzi wa 2022 uliibiwa na Ruto -- lakini bado anasema anahisi "kusalitiwa" na serikali. 

Odinga alichukua hali hii ya kuchanganyikiwa mitaani, na kuandaa maandamano ya siku 10 mapema mwaka huu ambayo yalisababisha vifo vya watu 50, kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Polisi Kenya yazuia maandamano ya upinzani

01:59

This browser does not support the video element.

Soma pia: Zaidi ya waandamanaji 300 washikiliwa na polisi nchini Kenya

Mazungumzo ya pande mbili yamekuwa yakifanyika ili kumaliza mkwamo huo, ingawa ajenda hiyo inajumuisha sio tu wasiwasi wa gharama ya maisha lakini kuundwa kwa ofisi mpya ya upinzani kumpa Odinga cheo rasmi na mitego mingine.

"Hivi sasa, Wakenya wengi wanaripotiwa kula mlo mmoja kwa siku, hivyo ikiwa majibu ya mazungumzo ya pande mbili hayana uhusiano na bei ya vyakula kushuka, hawatahisi kama ni ushindi," alisema mchambuzi wa masuala ya kisiasa Nerima Wako-Ojiwa.

Katika mwaka wake wa kwanza, Ruto amejijengea taswira katika jukwaa la kimataifa kama bingwa wa mazingira na mpigania mageuzi ya taasisi za utoaji mikopo duniani.

Wiki iliyopita, alikuwa mwenyeji wa wakuu wa nchi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano mkuu wa Tabianchi ambao ulivutia mabilioni ya uwekezaji wa nishati safi kwa Afrika.

Baadhi ya wakosoaji wamemshutumu Ruto kwa vipaumbele vinavyokinzana, kuandaa mikutano ya kilele na kusafiri nje ya nchi huku kile kinachojulikana kama "taifa la hustler" kikikaza mkanda wake.

Joseph Mwiti, mwongoza watalii mwenye umri wa miaka 32 na baba wa watoto wawili, alisema ni mapema mno kuhukumu na yuko tayari kumpa Ruto muda zaidi.

"Unapojenga nyumba, huwezi kuanza kuishi mara moja," alisema.

Chanzo: AFPE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW